Habari

Raila ateka baraka za wazee Mlimani

June 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WAIKWA MAINA

WAZEE wa jamii ya Wakikuyu wameapa kumtetea Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga dhidi ya shutuma kutoka kwa baadhi ya wanachama wa Jubilee katika ngome hiyo ya kisiasa ya Rais Uhuru Kenyatta.

Baraza la Wazee wa Jamii ya Wakikuyu lilisema Jumapili kuwa, wanasiasa wa ‘Tangatanga’, hasa kutoka eneo la Mlima Kenya na Bonde la Ufa ambao wamekuwa wakimshambulia Bw Odinga kwa ushirikiano wake na Rais Kenyatta wanatatiza juhudi za serikali kufanikisha ajenda ya maendeleo.

Kwa muda mrefu, wanasiasa hao wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakidai Bw Odinga alichangia kusambaratisha kwa chama chao.

Wengine hudai ushirikiano wake na Rais Kenyatta umefanya washukiwa wa ufisadi kupata mahali pa kujisitiri chini ya mwavuli wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Msemaji wa baraza hilo, Bw Peter Munga, alisema kelele za wanasiasa wa ‘Tangatanga’ hazifanikisha kampeni ya kupambana na ufisadi nchini.

Kulingana naye, badala ya kumshambulia Bw Odinga, viongozi hao wanafaa kupigania kuimarishwa kwa asasi tofauti za kuangamiza ufisadi nchini.

Alisema hayo baada ya Seneta wa Nakuru Susan Kihika na aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo kudai kuwa Bw Odinga ameshindwa kukemea ufisadi tangu aanze kushirikiana na Rais Kenyatta.

Wawili hao waliokuwa wakizungumza katika kituo kimoja cha runinga cha lugha ya Kikuyu walisema kuwa, Bw Odinga ambaye alikuwa katika mstari wa mbele kufichua sakata za ufisadi amenyamaza tangu handisheki yake na Rais Kenyatta mnamo Machi 2018.

“Ili kushinda zimwi la ufisadi nchini, tunahitaji upinzani wenye nguvu. Bw Odinga alinyamaza baada ya kufanya handisheki na Rais Kenyatta. Kiongozi yeyote anayeshukiwa kuhusika na ufisadi, sasa anaenda katika afisi ya Bw Odinga katika jumba la Capitol Hill kutakaswa,” akadai Seneta Kihika.

Bw Munga alisema tatizo kubwa linalokumba Serikali ya Rais Kenyatta ni kutokana na jinsi Dkt Ruto na wandani wake wanavyofuata mkondo tofauti na ule wa Ikulu.

“Naibu wa Rais Ruto amechukua baadhi ya viongozi wa Jubilee na sasa anaendesha serikali mbadala. Zana za uongozi wa nchi hii zilikabidhiwa Rais Kenyatta na wala si kwa Ruto,” akasema Bw Munga.

Wakati huo huo, alimtaka Rais Kenyatta aendelee kuwatimua viongozi wanaomkaidi wakiwemo mawaziri na maafisa wengineo katika idara za serikali akisema wao ndio wamekuwa wakihujumu ajenda yake ya maendeleo.

Bw Munga ambaye huwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Mlima Kenya alisema ni dhahiri kuwa Rais Kenyatta anataka kukumbukwa kwa kusaidia Kenya kustawi kimaendeleo hivyo hana budi kutimua yeyote anayemhujumu.