WASONGA: Hukumu itasaidia kukabili vita dhidi ya ufisadi nchini
Na CHARLES WASONGA
HUKUMU kali aliyopewa Mbunge wa Sirisia John Waluke na mshukiwa mwenzake Grace Wakhungu, imerejesha matumaini kwa Wakenya kwamba vita dhidi ya ufisadi vinaweza kufaulu nchini endapo havitaingiliwa kisiasa.
Katika uamuzi uliotajwa kama wa kihistoria, Hakimu wa mahakama ya ufisadi Grace Juma aliwatoza wawili hao faini ya jumla ya Sh2.2 bilioni au wafungwe gerezani kwa miaka saba, kila mmoja, kwa kupatikana na makosa ya wizi wa zaidi ya Sh313 milioni mnamo 2014.
Mahakama ilithibitisha kuwa wawili hao walipokea pesa hizo kutoka kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) baada ya kudanganya kuwa waliiuzia mahindi.
Hukumu hiyo imedhihirisha kuwa ikiwa mahakama zetu zitaruhusiwa kufanya kazi yao katika mazingira huru pasina kuingiliwa na maafisa wa serikali au wanasiasa wenye ushawishi mkubwa, ufisadi utatokomezwa nchini.
Nilifuatilia kwa karibu zaidi jinsi kesi hiyo ilivyoendeshwa na nikashawishika kwamba kando na mahakama, asasi zote zilihusika katika uchunguzi zilifanya kazi bila kuingiliwa kwa njia yoyote.
Bila shaka kutoingiliwa huku kwa asasi za uchunguzi, kama vile Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), kulipelekea Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuwasilisha kesi yenye ushahidi.
Uamuzi huo uliotolewa wiki jana Alhamisi usiku, umeonyesha kuwa mahakama zetu zina uwezo wa kuwaadhibu washukiwa wa ufisadi pasi na kuzingatia hadhi au vyeo vyao.
Kwamba mahakama zetu zina uwezo wa kuwahukumu hata “samaki wakubwa” endapo mahakimu na majaji watapewa ushahidi thabiti.
Inaridhisha kuwa licha ya mawakili Evans Ondieki na Danstan Omari kuomba Waluke apewe hukumu nyepesi kwa sababu yeye ni Mbunge mheshimiwa, ombi lao liligonga mwamba, sawa na kisingizio cha umri wa Bi Wakhungu (miaka 70).
Hukumu iliyotolewa na Bi Juma imeonekana kuiondolea idara ya mahakama lawama za kila mara kwamba ndio imekuwa ikuhujumu vita dhidi ya ufisadi kwa kuwaachilia washukiwa kwa kisingizio cha “ukosefu wa ushahidi wa kuhimili kesi.”
Muhimu zaidi ni kwamba hukumu hiyo sasa imeonekana kuwatia tumbojoto watu wengine mashuhuri wanaokabiliwa na kesi za ufisadi katika mahakama za humu nchini.
Wao ni watu kama vile; magavana Mike Sonko (Nairobi), Moses Kasaine (Samburu), magavana wa zamani Evans Kidero na Ferdinand Waititu pamoja na Mbunge wa Lugari Ayub Savula.
Watu kama hawa wajue kwamba sasa chuma chao ki motoni kwani kila mmoja wao anakabiliwa na tuhuma za kupora zaidi ya Sh20O milioni, pesa za umma.
Hukumu dhidi ya Waluke na Wakhungu imethibitisha kuwa taifa hili lina sheria tosha za kukabiliana na zimwi la ufisadi ambalo hufyonza takriban thuluthi moja ya jumla ya mapato ya taifa hili kila mwaka.
Sasa Wakenya wanasubiri kwa hamu kubwa uamuzi kuhusu kesi dhidi ya watu niliotaja hapo juu na wengine kama vile aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich na aliyekuwa Katibu wa wizara hiyo Kamau Thugge.