Mario Gomez astaafu baada ya kuisaidia VfB Stuttgart kurejea Bundesliga

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI matata wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani, Mario Gomez, ameangika rasmi daluga zake kwenye ulingo wa soka akiwa na umri wa miaka 34 baada ya kukisaidia kikosi chake cha awali cha VfB Stuttgart kurejea katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) msimu ujao.

Gomez aliwafunga bao la pekee la Stuttgart katika mechi iliyowashuhudia wakipokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Darmstadt mnamo Jumapili iliyopita.

Darmstadt walikamilisha mechi wakiwa na wachezaji 10 uwanjai baada ya Victor Palsson kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 67. Magoli yao yalimiminwa wavuni kupitia kwa Serdar Dursun, Matthias Bader na Tobias Kempe.

Licha ya kupoteza mchuano huo, Stuttgart ambao ni mabingwa mara tano wa taji la Bundesliga, bado walisalia katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Ujerumani (Bundesliga 2) kwa alama 58 huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na viongozi Arminia Bielefeld.

“Hicho kilikuwa kibarua change cha mwisho kambini mwa Stuttgart. Imekuwa ndoto yangu kustaafu nikivalia jezi za kikosi hiki, na hasa baada ya kuwapa kitu cha kujivunia,” akasema Gomez.

Gomez aliwajibishwa na timu ya taifa ya Ujerumani mara 78 kabla ya kustaafu soka ya kimataifa miaka miwili iliyopita.

Alianza kupiga soka ya kitaaluma kambini mwa Stuttgart mnamo 2001 na kukiongoza kikosi hicho kunyanyua ufalme wa Bundesliga mnamo 2006-07.

Alijiunga baadaye na Bayern Munich mnamo 2009 na kusaidia miamba hao wa soka ya Ujerumani kutia kibindoni mataji mawili ya Bundesliga na ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Alichezea baadaye Fiorentina (Italia), Besiktas (Uturuki) na VfL Wolfsburg (Ujerumani) kati ya 2013 na 2016 kabla ya kurejea Stuttgart mwanzoni mwa msimu wa 2017-18.

Tangu wakati huo, amewajibishwa na Stuttgart katika jumla ya mechi 70 na akapachika wavuni mabao 22.

Habari zinazohusiana na hii