• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Waziri Amina amtakia Kamworor afueni baada ya kugongwa na pikipiki mazoezini

Waziri Amina amtakia Kamworor afueni baada ya kugongwa na pikipiki mazoezini

Na GEOFFREY ANENE

WAZIRI wa Michezo, Amina Mohamed amemtakia Geoffrey Kamworor afueni ya haraka baada ya bingwa huyo mara tatu wa riadha za Nusu-Marathon duniani kugongwa na pikipiki Juni 25 akifanya mazoezi yake ya asubuhi kwenye barabara ya Kaptagat-Eldoret.

Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alitibiwa katika hospitali ya St Luke’s mjini Eldoret katika kaunti ya Uasin Gishu na kuruhusiwa kuendelea na matibabu kutoka nyumbani.

Katika ajali hiyo, mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 ya dakika 58:01 aliyoweka jijini Copenhagen nchini Denmark mwaka 2019, alijeruhiwa kichwani na katika kifundo chake.

Mwendeshaji wa pikipiki hiyo aliisimamisha na kumpeleka hospitalini alikolazwa na kufanyiwa upasuaji.

“Natakia mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 Geoffrey Kamworor afueni ya haraka anapotoka hospitalini. Nashukuru maafisa wa afya waliomhudumia kufuatia ajali hiyo,” alisema waziri huyo Juni 29 kwenye mtandao wake wa Twitter.

Majeraha hayo yanaweza kusababisha bingwa huyu wa New York Marathon mwaka 2017 na 2019 akose kutetea taji lake la Nusu-Marathon Duniani mjini Gdynia nchini Poland mnamo Oktoba 17 yasipopona haraka.

You can share this post!

COVID-19: Visa 120 vipya, wagonjwa 42 wapona na mmoja...

Real Madrid yafungua mwanya wa alama mbili kileleni mwa La...

adminleo