Michezo

Olunga aungana na Wakenya kutakia jagina Musa Otieno apone Covid-19

June 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MFUMAJI matata wa Kashiwa Reysol inayoshiriki Ligi Kuu ya Japan, Michael Ogada Olunga ametuma ujumbe wa kumtakia jagina Musa Otieno afueni ya haraka.

Otieno, ambaye alisakata soka yake katika klabu ya Tusker humu nchini na Santos ya Afrika Kusini, amelazwa hospitalini baada ya kuambukizwa Covid-19.

Baada ya kupokea habari za mchezaji huyo wa zamani wa Harambee Stars kwamba ana Covid-19, mshambuliaji Olunga alisema kwenye mtandao wa kijamii, “Natumai utapata kutabasamu tena bingwa. Afueni ya haraka shujaa.”

Otieno amekuwa katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya virusi vya corona tangu kisa cha kwanza cha maambukizi kiliporitiwa Machi 12. Inasemekana alipatikana na virusi hivyo wikendi ya Juni 27-28 na amelazwa katika hospitali ya Mbagathi kupokea matibabu.

Beki huyo mstaafu mwenye umri wa miaka 46 alichezea Kenya mechi 70 na kufunga mabao 12 kati ya mwaka 2003 na 2009 alipostaafu kuchezea taifa lake.

Olunga anajiandaa kurejea uwanjani hapo Julai 4 wakati J-League inavyofahamika Ligi Kuu ya Japan, itakapoanza tena baada ya kusimamishwa mwezi Machi kutokana na janga la Covid-19.

Timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande almaarufu Shujaa na Wakenya wengi tu wamemtakia Otieno afueni ya haraka. Kufikia Juni 30, Kenya imethibitisha visa 6,366 vya maambukizi ya corona na vifo 148.