ULIMBWENDE: Mwonekano mzuri wa uso wa mwanawake
Na MISHI GONGO
WANAWAKE huthamini sana mwonekano wa nyuso zao na ndiyo maana wengi hutumia muda mwingi na mali katika urembo ili wavutie.
Ili wapendeze, wang’are na kuondoa chunusi wengi wa wanawake hutumia bidhaa za kemikali ambazo huharibu zaidi ngozi za nyuso zao.
Japo wengi hupendelea kuwa na ngozi nyororo zenye mvuto, si wote waliobarikiwa na hali hiyo na hivyo inabidi kutumia bidhaa mbalimbali kujirembesha.
Baadhi ya bidhaa zinazouzwa madukani huwa na kemikali ambazo huharibu zaidi ngozi ndiposa wataalamu wa masuala ya ngozi hupendekeza bidhaa za kiasilia kutunza ngozi.
Pia hupendekeza mtu kuwa na mazoea ya kusafisha uso wake angalau mara mbili kwa siku ili kudhibiti kulundikana kwa uchafu unaosababisha uso kupata chunusi.
Kusafisha uso mwanamke anahitajika kuwa na skrabu. Skrabu huondoa ngozi iliyokufa na kutoa miba usoni.
Miongoni mwa skrabu za asilia ni kusinga uso au hata mwili mzima kwa kutumia skrabu ya unga wa pojo zilizosagwa.
Manufaa yake ni kuwa husafisha uso na kuondoa weusi unaosababishwa na kuchomwa na jua.
Pia unaweza kutengeza skrabu au singo kwa kuchanganya bizari, karafuu na asali au mafuta ya karafuu.
Faida ya singo hiyo husaidia kuiweka ngozi yako kuwa imara, huondoa uchovu na kuchangamsha mwili, huifanya ngozi yako kuwa laini na nyororo bila chunusi na husaidia kuifanya ngozi isizeeke haraka.
Aidha unaweza kutumia asumini kavu na mawaridi yaliyochanganywa na rose water kujisinga.
Singo hiyo hulainisha ngozi na kuondoa mikunjo. Pia huondoa weusi unaosababishwa na kuchomwa na jua.
Baada ya kusinga uso, mwanamke anaweza kutumia mafuta safi ya nazi au karafuu katika kuifanya ngozi ya uso wake kung’aa na kuwa na mvuto.