WASONGA: Kuwe na mazingira faafu kabla shule kufunguliwa
Na CHARLES WASONGA
KAULI ya Waziri wa Elimu, George Magoha kwamba, huenda shule zikafunguliwa Januari mwaka ujao inaonyesha kuwa, serikali haijaandaa mazingira faafu ya kuzuia maambukizi ya virusi hivyo shuleni.
Na huu mwenendo wa Profesa Magoha kutoa kauli tofauti kila mara kuhusu suala hili muhimu unawakanganya wadau katika sekta ya elimu, haswa wazazi ambao wanakabiliwa na makali ya janga la Covid-19.
Wazazi walikuwa wametarajia kwamba, shule za msingi na za upili zingefunguliwa kuanzia Septemba alivyoahidi Rais Uhuru Kenyatta kwenye hutoba yake kwa taifa Juni 6.
Lakini inavunja moyo kwamba, sasa Profesa Magoha anadai shule haziwezi kufunguliwa Septemba eti kutokana na ongezeko la maambukizi ya Covid-19 nchini.
Ni juzi tu ambapo Waziri huyo aliwaambia Wakenya kuwa shule zitakapofunguliwa mwezi huo, darasa moja litakuwa na wanafunzi 20 pekee. Lakini hakuelezea mikakati ambayo wizara yake imeweka kufanikisha mpango huo; kama vile ujenzi wa madarasa zaidi au uajiri wa walimu zaidi.
Japo Rais Kenyatta alimwagiza Waziri Magoha kupanga vikao na wadau kwa ajili ya kuandaa mwongozo utakaowezesha shule kufunguliwa kwa awamu huku kanuni za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona zikizingatiwa, serikali haijatoa fedha za kugharamia mpango huo.
Hii ina manaa kuwa, Rais alitoa maagizo pasina kuyaandamanisha na rasilimali za kufanikisha utekelezaji wa maagizo hayo. Taswira inayojitokeza hapa ni ya serikali ambayo haitilii maanani masomo ya watoto ilhali hii ni mojawapo ya haki za watoto kulingana na kipengele cha 43 cha Katiba.
Inaudhi kwamba, mapema Mei, Waziri Magoha alibuni kamati maalum ya wadau katika sekta ya elimu iliyotwikwa jukumu la kukusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu mwongozo wa kuwezesha kufunguliwa kwa shule.
Kamati hiyo iliyoongozwa na mwenyekiti wa Taasisi ya Kutayarisha Mitaala (KICD) Sarah Ruto ilipendekeza kuwa, shule zifunguliwe, kwa awamu kuanzia Septemba.
Aidha, kamati hiyo ilipendekeza mitihani ya kitaifa; ule wa Darasa la Nane (KCPE) na ule wa Kidato cha Nne (KCSE), iahirishwe hadi mwaka 2021.
Kulingana na kamati hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Elimu ilifaa kuhakikisha shule zimejiandaa kufanikisha utekelezaji wa kanuni za Wizara ya Afya za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Kwa mfano, serikali ilipasa kutoa fedha za kufadhili mpango wa kuweka maji katika shule zote kando na kujenga madarasa na mabweni zaidi.
Aidha, serikali ilipasa kutoa fedha za kuajiri walimu zaidi ikizingatiwa kuwa, kuna uhaba wa takriban walimu 130, 000 katika shule zote za msingi na za upili nchini.
Kwa kufeli kutekeleza mapendekezo kama haya, ni wazi kuwa serikali haichukulii kwa uzito masomo ya watoto wa taifa hili ambayo sasa wanapitia madhila mengi nyumbani.
Watoto wa kike wanatungwa mimba kiholela huku wengine wakiozwa mapema. Na wavulana wanajiunga na magenge ya ujambazi.
Serikali ikome kuingiza mzaha katika suala hili la masomo ya watoto kwani wao ndio rasilimali muhimu zaidi kwa taifa hili.