• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 4:55 PM
Muhiddin asema viwango vya ukufunzi wa soka nchini vimeimarika

Muhiddin asema viwango vya ukufunzi wa soka nchini vimeimarika

Na CHRIS ADUNGO

MKUFUNZI Twahir Muhiddin amesema viwango vya ukocha humu nchini vitaimarika zaidi iwapo mafunzo ya sasa yanayodhaminiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa ushirikiano na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) yataendelezwa katika viwango mbalimbali kote nchini.

Katika kipindi cha mika minne iliyopita, zaidi ya makocha 3,000 wamepokeza mafunzo ya bure katika viwango vya mbalimbali hadi kufikia kile cha Leseni ya ‘C’ ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Mbali na kuwakuza wakufunzi kitaaluma, lengo jingine la mafunzo hayo ni kuboresha viwango vya ukufunzi miongoni mwa makocha ambao kwa sasa huwapa wachezaji malezi ya soka katika madaraja mbalimbali.

“Ni mradi utakaohakikisha kwamba wanasoka chipukizi kutoka mashinani wananolewa na makocha waliohitimu na kuelewa sheria zote za mchezo. Isitoshe, mafunzo huyo yanakusudia kuziba pengo la ukufunzi kati ya chipukizi wa viwango mbalimbali na wanasoka wa timu za taifa na klabu,” akasema Muhiddin.

Muhiddin anashikilia kwamba kukosekana kwa majukwaa ya kuwapa makocha mafunzo ya kitaaluma, ni kati ya mambo ambayo yamenyima idadi kubwa ya wakufunzi fursa mbalimbali za kudhibiti mikoba ya vikosi vya haiba kubwa humu nchini na hata mataifa ya kigeni.

Mtazamo wa Muhiddin unaungwa na wakufunzi wa FIFA kwa upande wa soka ya wanawake, Dorcas Moraa na Caroline Wanjala ambao wamekiri kwamba hatua ya FKF kuondoa ada ya Sh3,000 kwa Wakenya kujisajilisha kwa mafunzo ya ukocha imevutia sasa idadi kubwa ya wadau ambao watazidisha ushindani na kuinua viwango vya ukufunzi.

You can share this post!

Mkuu wa huduma za feri akatazwa kutumia eneo la VIP...

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 247 idadi jumla...

adminleo