Habari

Waluke aomba aruhusiwe kushiriki mijadala ya bunge kwa Zoom akiwa jela

July 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Sirisia John Waluke anayetumikia kifungo miaka 67 amewasilisha ombi la kipekee katika Mahakama Kuu aruhusiwe kushiriki katika mijadala ya bunge akiwa gerezani kupitia ama Skype au Zoom.

Waluke anaomba Mahakama Kuu imwamuru msimamizi wa gereza la Viwandani Nairobi anakozuiliwa amtengee chumba maalum kitakachowekwa mitambo ya kumwezesha kushiriki katika mijadala ya bunge.

Waluke aliyefungwa pamoja na mkurugenzi mwenzake katika kampuni ya ya Erad Supplies & General Contracts Limited Grace Sarapay Wakhungu Alhamisi iliyopita, anasema wakazi wa Sirisia wanahitaji kuwakilishwa bungeni.

Waluke atakuwa mfungwa wa kwanza kukubaliwa kuendeleza kazi yake akiwa kifungoni ikiwa ombi lake litakubaliwa.

Kwa mujibu wa sheria, mtu akifungwa anakoma kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa vile hali yake huwa imebadilika kutoka mtu huru na kuwa mfungwa ama mahabusu chini ya ulinzi wa askari jela.

Wakhungu alihukumiwa kifungo cha miaka 69 jela.

Bila kusita, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma DPP atapinga ombi hili la Waluke kupewa huduma spesheli anapotumikia kifungo hicho cha miaka 67 jela.

Wote walisukumiwa vifungo hivyo na hakimu mkuu Elizabeth Juma aliyeamuru watumikie kifungo kimoja baada ya kingine.

Kupitia kwa wakili Samson Nyaberi, Waluke anaomba mahakama kuu “itilie maanani maslahi ya wakazi wa eneo la uwakilishi bungeni la Sirisia kisha iamuru atengewe chumba awe akiwashughulikia kutoka gerezani.”

Akitoa mukhutasari wa rufaa hiyo iliyo na aya zaidi ya 40, Bw Nyaberi alifichua tayari amemwandikia Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi akimwarifu kuhusu rufaa aliyokata Waluke ndipo kiti cha Sirisia kisitangazwe wazi akikosa kuhudhuria vikao vinane.

“Tulimwandikia barua Spika wa Bunge la Kitaifa na kuandamanisha nakala ya rufaa tuliyowasilisha ndipo kiti cha Sirisia kisitangazwe wazi,” Bw Nyaberi ameeleza Taifa Leo katika Mahakama Kuu ya Milimani Nairobi Ijumaa.

Bw Nyaberi na mawakili wengine watano wameukosoa uamuzi wa hakimu mkuu Bi Elizabeth Juma aliyewahukumu Waluke na Grace wakisema “hakuzingitia ushahidi wote uliowasilishwa mbele yake na washtakiwa.”

Bw Nyaberi alisema wanasubiri kupokea nakala zote za kesi hiyo ndipo wajue jinsi ya kuubomoa wakilenga kuachiliwa kwa wawili hao.

Pia alisema amewasilisha ombi Waluke aachiliwe kwa dhamana kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa rufaa aliyokata.

“Tutaomba Mahakama Kuu imwachilie mfungwa huyu kwa dhamana aendelee kuhudhuria vikao vya bunge kwa vile sasa eneo la uwakilishi bungeni la Sirisia halina mwakilishi,” Bw Nyaberi alisema.

Alisema watategemea umri mkubwa wa mbunge huyo kuirai korti imwachilie kwa dhamana asiambukizwe Covid-19 akiwa gerezani.

Akimtetea Waluke asisukumiwe kifungo cha gerezani, Nyaberi alisema mwanasiasa huyo anaugua maradhi ya kisukari.

Mawakili watang’ang’ana kifungo hicho cha miaka 67 kipunguzwe hadi miaka saba

Mawakili hao wanasema kulingana na ushahidi uliowasilishwa kortini sheria za uhalifu hazingelitumika kumfungulia mashtaka mwanasiasa huyo kwa vile suala la kuagiza mahindi tani 40,000 kutoka ng’ambo kwa idhini ya NCPB lilikuwa suala la kibiashara.

Wote wawili walikabiliwa na shtaka la kuilaghai Halmashauri ya Nafaka na Mazao (NCPB) Sh297,386,505

Shtaka la pili dhidi ya wote wawili lilisema waliifuja NCPB Sh13,364,671

Shtaka la tatu lilisema walifuja NCPB dola za Kimarekani 24,032 (Sh2,403,200).

Grace alikuwa ameshtakiwa peke yake kwamba alitumia stakabadhi ya kughushi kama ushahidi katika kesi iliyotatuliwa na mpatanishi kati ya Erad na NCPB.

Akitoa hukumu Bi Juma aliwatoza faini ya lazima ya Sh500,000 kwa kosa la kupokea pesa kwa njia ya undanganyifu kila mmoja ama kila mmoja atumikie kifungo cha miaka mitatu gerezani.

Bi Juma alisema kwa mujibu wa kifungu cha sheria nambari 48 cha sheria za ufisadi kila mmoja atalipa faini ya Sh1,189,546,020 ama kutumikia kifungo cha miaka saba gerezani kwa kosa la kusababisha NCPB kupoteza Sh297,386,505

Katika shtaka la tatu lilikuwa la kupokea Sh13,364,671 kila mmoja alitozwa faini ya Sh500,000 ama kutumikia kifungo cha miaka mitatu gereza.

Mbali na faini hiyo kwa kusababisha NCPB kupoteza Sh13,364,671 kila mmoja alitozwa faini ya Sh26,729, 342 ama kutumikia kifungo cha miaka saba gerezani.

Kwa kupokea dola za Kimarekani 24,032 (Sh2,402,200) kila mmoja alitozwa faini ya Sh4,806,400 ama watumikie kifungo cha miaka saba.

Waluke atalipa faini ya Sh1,211,581,762 ama atumikie kifungo cha miaka saba gerezani.

Grace atalipa faini ya Sh1,211,781,762 baada ya faini yake kuongezeka kwa vile alitozwa faini ya Sh200,000 kwa kutoa ushahidi wa uongo na kughushi stakabadhi za tenda.