Michezo

Messi achoshwa na Barcelona

July 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

NAHODHA na mshambuliaji matata mzawa wa Argentina, Lionel Messi, 33, amesema amechoka na Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Kauli ya Messi ambaye ametawazwa mwanasoka bora duniani mara sita, inatarajiwa sasa kufufua azma ya Manchester City, Inter Milan na Juventus kuziwania huduma zake.

Katika mahojiano yake na redio ya Cadena Ser nchini Uhispania, Messi amefichua kwamba amesitisha mazungumzo kuhusu uwezekano wa kurefushwa kwa mkataba wake uwanjani Camp Nou na kukiri kutamaushwa na tetesi za mara kwa mara zinazomhusisha na kusuasua kwa Barcelona na mizozo ya mara kwa mara kati ya wachezaji na vinara wa benchi ya kiufundi.

“Nimechoshwa na madai kwamba mimi ndiye niayeendesha klabu ya Barcelona. Nimechoshwa na kauli za watu kwa mimi ndiye huajiri na kuwatimua makocha wa Barcelona. Nimechoshwa na tetesi kwamba mimi ndiye huamua ni mchezaji yupi anafaa kusajiliwa na Barcelona, nani anastahili kuchezeshwa katika kikosi cha kwanza na yupi anafaa kutiwa mnadani.”

“Inatamausha sana kila mara unapolaumiwa kwa matokeo duni ya kikosi na makosa ya klabu katika soko la uhamisho wa wachezaji,” Messi alinukuliwa huku akidokeza uwezekano wa kuagana na miamba hao wa soka ya La Liga mwishoni mwa muhula ujao wa 2020-21.

“Madai ya uongo dhidi yangu yametolewa pia kuhusiana na mchezaji Antoine Griezmann. Kwamba mimi ndiye nilishinikiza Barcelona kumsajili kutoka Atletico Madrid mwanzoni mwa msimu huu. Sasa zipo tetesi kwamba mimi simtaki tena Griezmann uwanjani Camp Nou.

“Ukweli ni kwamba Griezmann alijiunga nasi kwa nia ya kufufua makali ya Barcelona waliohisi kwamba ndiye atakayekuwa kizibo cha Neymar aliyeyoyomea PSG. Ingawa nyota ya Griezmann bado haijaanza kung’aa kabisa Barcelona, nimekuwa nikishiriana sana na Luis Suarez kumsaidia kuzoea mazingira ya Camp Nou.”

“Nimewahi pia kuhusishwa na maamuzi ya kutimuliwa kwa kocha Tata Martino na kuajiriwa kwa Quique Setien. Nimesikia na kusoma katika vyombo vya habari kwamba sasa mimi na Setien hatuelewani na nitaka usimamizi wa Barcelona umfute kazi. Huo ni uongu mtupu.”

“Ieleweke kwamba mimi si mtu wa aina hiyo. Sijigambi kutokana na ufanisi wangu kitaaluma wala mshahara mnono ninaolipwa. Kusema kweli, hakuna maamuzi yoyote ninayoweza kufanya kambini mwa Barcelona isipokuwa pale mtazamo wa wachezaji huhitajika. Nami huwasilishia usimamizi kauli ambayo huwa ni zao la kushauriana na wachezaji wenzangu wote ambao nawaheshimu sana.”

Ni mwezi mmoja tu umepita tangu wanachama sita wa Bodi ya Usimamizi ya Barcelona kujiuzulu na baadhi ya wanasoka wa kikosi hicho kumwelezea Rais Josep Bartomeu Maria kwamba hawajaridhishwa kabisa na namna ambavyo klabu hiyo inaendeshwa.

Bartomeu amelaumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha, kushindwa kumrejesha Neymar uwanjani Camp Nou na kumfuta kazi kocha Ernesto Valverde aliyeanza kufufua makali ya Barcelona.

Bartomeu anatazamiwa kubanduka mwishoni mwa 2021 na nafasi yake kutwaliwa na Victor Font ambaye anapigiwa upatu wa kushinda uchaguzi ujao wa urais wa Barcelona.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, Barcelona wanatazamiwa kumfuta kazi kocha Setien mwishoni mwa msimu huu na nafasi yake kutwaliwa na kiungo wa zamani wa Barcelona, Xavier Hernandez.

Kikosi hicho ambacho kwa sasa kinawania huduma za mvamizi Lautaro Martinez kutoka Inter, kinashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la La Liga kwa alama 70, nne nyuma ya Real Madrid.