Vardy afikisha mabao 100 katika soka ya EPL
Na CHRIS ADUNGO
JAMIE Vardy alifunga bao lake la 100 na 101 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kuwezesha Leicester City kuwapepeta Crystal Palace 3-0 uwanjani King Power.
Ushindi huo uliwaweka Leicester pazuri zaidi jedwalini kadri wanavyolenga kukamilisha kampeni za muhula huu katika nafasi ya nne na kujikatia tiketi ya kunogesha kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.
Kelechi Iheanacho aliwafungulia Leicester ukurasa wa mabao kunako dakika ya 49 kabla ya Vardy kushirikiaa vilivyo na Harvey Barnes katika dakika ya 77 na kufunga goli lake la 100.
Baada ya kushindwa kutikisa nyavu za wapinzani wao katika mechi tatu mfululizo tangu kurejelewa kwa kivumbi cha EPL mnamo Juni 17, Vardy alipachika wavuni bao lake la pili mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa Palace na kumwacha hoi kipa Vicente Guaita.
Leicester walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakiwa na ulazima wa kusajili ushindi ili kuepuka hatari ya kupitwa na Manchester United walioanza kuusoma mgongo wao kwa karibu baada ya kusajili sare mbili na kupoteza mara moja katika mechi tatu za awali.
Kwa sasa wanajivunia alama 58, tatu zaidi kuliko Man-United wanaofunga mduara wa nne-bora kileleni mwa jedwali.
Vardy alifunga bao lake la 100 katika EPL baada ya kusakata jumla ya mechi 206.
Orodha ya wanasoka waliowahi kufunga mabao 100 katika EPL haraka zaidi inaongozwa na aliyekuwa mshambuliaji wa Newcastle United, Alan Shearer aliyefikia ufanisi huo baada ya michuano 124 pekee.
Hadi alipoingia katika sajili rasmi ya Leicester, Vardy alikuwa pia amewachezea Stocksbridge Park Steels, Halifax na Fleetwood ambavyo ni vikosi vya madaraja ya chini katika soka ya Uingereza.
Baada ya kufunga mabao 17 kutokana na mechi 19 kabla ya mwisho wa mwaka wa 2019, kisu cha makali ya Vardy kilisenea pakubwa katika mwaka huu wa 2020 ambao umemshuhudia akipachika wavuni magoli mawili pekee kutokana na michuano 10.
Anapolenga kufunga mabao zaidi na kutawazwa mfungaji bora wa EPL msimu huu, Vardy kwa sasa anajiandaa kuwaongoza Leicester kuvaana na Arsenal uwanjani Emirates mnamo Jumanne ya Julai 7, 2020 huku Palace wakiwaalika Chelsea ugani Selhurst Park.
WANASOKA WA KWANZA KUFIKISHA MABAO 100 KATIKA EPL
Jina Idadi ya Mechi
Alan Shearer 124
Harry Kane 141
Sergio Aguero 147
Thierry Henry 160
Ian Wright 173
Robbie Fowler 175
Les Ferdinand 178
Michael Owen 185
Andy Cole 185
Robin van Persie 197