• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 2:13 PM
JAMVI: Mudavadi ‘manyanga’ kila mrengo wamtaka kambini

JAMVI: Mudavadi ‘manyanga’ kila mrengo wamtaka kambini

Na MWANGI MUIRURI

MUSALIA Mudavadi kwa sasa ndiye ‘mrembo’ wa kisiasa anayewindwa kwa udi na uvumba na mirengo yote miwili mikuu ya kisiasa nchini katika kipute cha urais 2022.

Hadi sasa, vita vya urais katika uchaguzi wa 2022 vinaonekana kuwa kati ya Naibu Rais, Dkt William Ruto na waziri mkuu wa zamani, Bw Raila Odinga.

Raila anategemea uungwaji mkono wa Rais Uhuru Kenyatta ambaye baada ya kupatana naye mnamo Machi 2018, kwa pamoja, wamewanasa Gideon Moi (Kanu), Isaac Ruto (Chama Cha Mashinani) na Kalonzo Musyoka (Wiper) katika mrengo mmoja.

Karata ya muungano huo inaonekana kulenga kumtenga Dkt Ruto na kumgeuza kuwa mdhaifu ambaye ataangaziwa kama mpweke wa kisiasa ambaye hataki uwiano na umoja wa kitaifa, ili akataliwe kwa kura za 2022.

Kwa upande wake, Dkt Ruto ameonekana kutochoka kuhepa mipigo kwani anaonekana kuwa mbioni kujipa nafasi ya 2022 dhidi ya muungano huo unaompinga.

Kwa mujibu wa aliyekuwa mbunge wa Maragua, Bw Elias Mbau, siasa za Dkt Ruto zitategemea pakubwa jinsi atakavyounda mrengo wake wa kumenyana na muungano wa Rais na Raila.

“Ususi wa mrengo wake lazima uzingatie idadi za watu kwa kuwa muungano wa UhuRaila ni mrengo ambao umejengwa ukilenga kuteka kura zote za kimaeneo. Naye Dkt Ruto ana kibarua hapa lakini ninamdokezea tu ajaribu kumnasa Mudavadi,” asema.

Anasema kuwa kumpata Mudavadi kutamfaa pakubwa katika vita vya kisaikolojia lakini si hasa kwa kumfaa kwa kura.

“Mudavadi leo hii akitangaza kuwa anamuunga mkono Dkt Ruto, kutakuwa na msisimko wa kisiasa hapa nchini,” asema.

Anaongeza: “Aidha, ikiwa Mudavadi ataamka leo hii atangaze kuwa anamuunga mkono Raila Odinga, kutakuwa na msisimko pia.”

Taswira hiyo inakuonyesha jinsi Mudavadi alivyorembeka kisiasa kiasi kwamba anabishaniwa hadharani na Ruto na Raila.

Naye kwa kuelewa thamani yake kisiasa, amejishasha kwelikweli akiwahepa ‘wanaomchumbia’ kiasi kwamba vyombo vya habari vimeripoti jinsi hata Rais Kenyatta ‘anavyomchumbia’ ajiunge naye ndani ya serikali.

Rais anasemekana kuwa ‘anamchumbia’ Mudavadi ili amnyime Dkt Ruto ushawishi katika jamii ya ‘Mulembe’ (Magharibi) na katika uchaguzi wa 2022, awe rahisi kushindwa.

Lakini mbona iwe Mudavadi anawindwa hivi? Ni urembo gani huu ameonekana kuwa nao kiasi hata anachumbiwa kwa kuahidiwa nafasi za kazi katika baraza la mawaziri na mashirika ya kiserikali?

Mbunge wa Maragua, Mary wa Maua anasema kuwa urembo wa Mudavadi ni kura za eneo la Magharibi. Wa Maua anasema kuwa mwenye kibarua kigumu cha kupata ufuasi wa Abaluhya ni Dkt Ruto kwa kuwa Raila amekuwa hata akimshinda Mudavadi katika kura ya urais katika jamii hii ya ‘Mulembe’.

Anasema kuwa kwa sasa Raila akiwa ndani ya serikali na ambapo anashirikiana na Rais Uhuru, kura za Mlima Kenya na Nyanza zina uwezekano mkuu wa kumponyoka Dkt Ruto.

“Ndiyo sababu ninasema Dkt Ruto ndiye ako na mlima wa kukwea wala sio Rais na washirika wake akiwemo Raila,” asema.

TF Body text: Hata hivyo, mhadhiri wa somo la siasa Gasper Odhiambo anasema thamani ya Mudavadi katika kinyang’anyiro cha 2022 haijang’amuliwa kwa undani na wengi.

 

You can share this post!

Presha yapanda kambi ya Ruto

JAMVI: Ushirika mpya wa Muthama na Kibwana mwiba kwa Kalonzo

adminleo