Makala

ULIMBWENDE: Vitu vya asili unavyoweza kutumia usoni bila madhara yoyote

July 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MARGARET MANA

[email protected]

BADALA ya kutumia vipodozi vikali ambavyo wakati mwingine huweza kusababisha maradhi kama saratani kwa sababu ya kemikali zilizonazo, ni vyema ukatumia vipodozi vya asili ambavyo ni rafiki kwa ngozi yako.

Hata hivyo aina yoyote ya ngozi ni nzuri ilimuradi isiwe na harara, upele au mabaka.

Watu weusi na weupe wasipozifanyia ngozi zao matunzo ni lazima ziharibike na zipoteze mvuto.

Jinsi ya kuifanya ngozi yako iwe na weupe wa kipekee kwa kutumia vitu vya asili ambavyo hupatikana jikoni mwako, tena kwa urahisi.

Ili kuing’arisha ngozi yako, unaweza kuvitumia vitu kama vile;

Limau

Limau linaweza kuufanya uso wako ukapata weupe wa kipekee na kwa wale wenye ngozi nyeusi wakawa wang’aavu.

Kata limau nusu. Ile nusu nayo ikate nusu, hivyo utapata robo.

Sugua limau katika uso wako na uruhusu juisi yake iingie katika ngozi yako.

Baada ya kufanya hivyo, acha juisi hiyo ibaki usoni kwa robo saa.

Osha uso wako kwa maji ya moto. Fanya hivyo angalau mara mbili kwa wiki, na utaona mabadiliko.

Asali na maziwa ya unga

Chukua kikombe, weka maziwa ya unga kijiko kimoja, asali kijiko kimoja na juisi ya limau nusu kijiko. Changanya kisha paka usoni na usugue taratibu. Acha usoni kwa dakika 15 na kisha osha taratibu kwa maji fufutende.

Utayaona matokeo baada ya muda mfupi.

Nyanya na unga wa mahindi

Chukua nyanya moja, isage kasha changanya na unga wa mahindi.

Jaribu kuufanya mchanganyiko wako mwepesi ili upakike na ukae usoni.

Sugua uso wako kwa mchanganyiko huo na uache ukae usoni kwa dakika 20.

Mchanganyiko wa matunda

Chukua tango, nanasi na papai bichi; visage.

Mchangayiko laini utakaopatikana hapo ndiyo dawa yako.

Usugue uso wako taratibu kutoka chini yaani kidevu ni kwenda juu.

Uache ukae usoni kwa dakika 20 kisha osha kwa maji ya baridi.