Makala

AFYA: Kitendawili kuhusu usahihi wa vipimo, ingawa sio Kenya pekee

July 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

WIZARA ya Afya imekiri kuwa baadhi ya maabara zimekuwa zikitoa matokeo ya kupotosha kuhusu virusi vya corona humu nchini.

Katibu Msaidizi (CAS) wa Wizara ya Afya Rashid Aman, Jumatano iliyopita, alikiri kuwa kuna uwezekano kwamba baadhi ya maabara ambazo zimeidhinishwa kupima virusi vya corona zimekuwa zikitoa matokeo yasiyo sahihi.

Hiyo inamaanisha kuwa kati ya watu karibu 8,000 ambao wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona humu nchini baadhi yao hawana na walijumuishwa kutokana na makosa katika vipimo.

Kadhalika, kuna uwezekano kuwa wengine waliopimwa na kupatikana bila virusi vya corona, wanavyo na wanaendelea kuvieneza kwa wengine.

Wizara ya Afya imeonya kuwa maabara zitakazopatikana na hatia ya kutoa matokeo ya kupotosha zitachukuliwa hatua ya kisheria.

Kulingana na Dkt Aman, usahihi wa matokeo hutegemea mbinu ya usafirishaji na muda ambao sampuli zilizochukuliwa kwa watu zinanakaa kabla ya kufanyiwa vipimo.

“Sampuli zikicheleweshwa kupimwa zinaweza kutoa matokeo tofauti. Iwapo sampuli zitahifadhiwa vyema, zinaweza kutoa matokeo sahihi hata baada ya wiki mbili. Lakini zikihifadhiwa ovyo ovyo zitatoa matokeo ya kupotosha,” akasema.

Wizara ya Afya mwezi uliopita ilifichua kuwa vifaa feki vya kupima virusi vya corona tayari vimeingia na vinauzwa humu nchini.

Mbunge wa Kiambu ya Kati Jude Njomo wiki iliyopita alifika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Afya akilalamika kuwa familia yake ililazimika kumzika mama yao Margaret Njomo kwa haraka baada ya kufahamishwa na wizara ya Afya kuwa alikuwa na virusi vya corona.

Kulingana na Njomo, mwendazake alikuwa amethibitishwa kuwa hakuwa na virusi vya corona.

Lakini baadaye wizara ya Afya iliwaletea matokeo tofauti yaliyothibitisha kuwa mama yao alikuwa na virusi vya corona.

Sampuli zilipopimwa tena katika Hospitali ya Nairobi matokeo yalikuwa tofauti na yale ya Wizara ya Afya.

Lancet ni miongoni mwa maabara ambazo zimekuwa zikidaiwa kutoa matokeo ya kupotosha ya virusi vya corona.

Lakini Mkurugenzi Mtendaji wa Lancet Afrika Mashariki Dkt Ahmed Kalebi anasema kuwa matokeo yanaweza kutofautiana kutoka maabara moja hadi nyingine kwa kutegemea kiwango cha virusi katika sampuli inayopimwa.

“Mashine tunazotumia katika maabara zetu zina uwezo wa kutambua hata kiasi kidogo cha virusi vya corona ambavyo huenda vikakosa kubainishwa katika maabara nyingine,” anasema Dkt Kalebi.

Wizara ya Afya imekuwa ikishauri Wakenya kutumia vifaa vilivyoidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Wataalamu wa afya wanahofia kuwa huenda vifaa hivyo feki vinavyouzwa humu nchini vimepenyezwa katika maabara zilizoidhinishwa kupima virusi vya corona.

“Wakenya hawafahamu tofauti kati ya vifaa feki na vile vilivyoidhinishwa na shirika la WHO. Serikali inafaaa kufanya uchunguzi ili kunasa maabara zinazotumia vifaa feki,” anasema Bw Paul Ochieng, mtaalamu wa masuala ya maabara.

Utata kuhusu usahihi wa matokeo pia umeripotiwa katika mataifa mbalimbali duniani.

Utafiti uliofanywa nchini Amerika ulibaini kuwa vifaa ambavyo vimekuwa vikitumiwa kupima virusi vya corona wafanyakazi wa Ikulu ya White House na wageni wanaotaka kukutana na Rais Donald Trump, havitoi matokeo sahihi kwa asilimia mia.

Mamlaka ya Kudhibiti Ubora wa Vyakula na Dawa nchini Amerika (FDA) wiki iliyopita ilisema kuwa imepokea zaidi ya malalamishi 120 kuhusu matokeo ya kupotosha yanayotolewa na vifaa vya kupima corona vilivyotengenezwa na kampuni ya Abbot Laboratories ambavyo hutumiwa katika Ikulu ya White House.