• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Haihalisi kutumia neno ‘fuatia’ kwa maana ya chanzo cha jambo fulani

Haihalisi kutumia neno ‘fuatia’ kwa maana ya chanzo cha jambo fulani

NA ENOCK NYARIKI

Baadhi ya watu hulitumia neno ‘fuatia’kwa maana ya chanzo au asili ya jambo fulani kama vile ugomvi, kisa, mkasa, tukio au kadhia yoyote.

Utawasikia wakisema: ‘Alimwangamiza mpenzi wake kufuatia mzozo wa kinyumbani’. Kauli kama hizi zi tele miongoni mwa wanahabari wazembe wasiopenda kufanya utafiti ili kuelewa maana ya baadhi ya maneno kabla ya kuyatumia kwenye taarifa.

Kauli ya kutendea ya kitenzi fuata ni fuatia. Hivyo ndivyo inavyojitokeza katika toleo la awali la Kamusi ya Kiswahili Sanifu na katika kamusi za punde zaidi za Kiswahili.

hivyo, lipo neno jingine linaloweza kuundwa kutokana na kitenzi tulichokitaja katika kauli hiyo moja. Neno hilo ni fuatilia. Kitenzi fuatilia kina maana ya kuchunguza au kuangalia kwa makini mwenendo wa mtu, kitu au jambo. Maana ya pili na ambayo imejikita katika tasnia ya uanahabari ni kuchunguzachunguza taarifa fulani kwa lengo la kupata utondoti au upya wa matukio.

Ijapokuwa maana ya kitenzi fuatilia haionekani kuhusiana kwa vyovyote na maana za kitenzi fuata, kuna uwezekano mkubwa kwamba kitenzi fuata ndicho kilichokizaa hiki cha kwanza.

Ushahidi wa kwanza tunaoweza kuutumia kulithibitisha jambo hilo ni kule kukosekana kwa kitenzi fuatilia katika toleo la awali la Kamusi ya Kiswahili Sanifu.

Tofauti na kamusi za punde zaidi ambapo kauli mbalimbali za baadhi ya vitenzi zinashughulikiwa kama maneno huru, kwenye toleo la awali la Kamusi ya Kiswahili Sanifu, maneno yote yaliyotokana na vitenzi fulani yalishughulikiwa chini ya kauli mbalimbali za vitenzi hivyo.

Nitaishughulikia hoja hii kwa kina katika makala tofauti ila katika makala haya tujibane kwenye kitenzi fuatia.

Maana ya kitenzi fuatia ni kuenda nyuma ya mtu au kitu kingine. Hakika, kuna tofauti finyu kimaana baina ya fuatia na fuata. Maana ya kitenzi hiki cha pili inaelezewa kwamba ni enda au kuja nyuma au baadaye.

Jambo moja ambalo ni muhimu kulifahamu kufikia hapa ni kuwa kwenye kamusi, kauli ya kutendea ya fuatia haijibainishi waziwazi. Badala yake, kitenzi chenyewe kinashiriki maana na kile kilichokizaa; yaani fuata. Hata hivyo, haimaanishi kuwa kitenzi fuatia hakiwezi kutumiwa kwa maana ya kutenda kwa niaba ya mtu mwingine.

Alhasili, neno fuatia halipaswi kutumiwa kwa maana ya chanzo cha jambo fulani. Iwapo nia ya mzungumzaji ni kueleza kuwa tukio fulani limesababishwa na jingine au ni kichocheo chake, kitenzi ‘tokana’ na kiunganishi ‘na’ vinapaswa kutumiwa kwa maana hiyo.

Kwa hivyo, tunapaswa kusema, ‘Alimwangamiza mpenzi wake kutokana na mzozo wa kinyumbani’. Kiunganishi ‘kwa sababu’ pia kinaweza kutumiwa katika mazingira hayo.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Jack Otiya, mwandishi chipukizi na mwalimu...

Makanisa na misikiti kufunguliwa Julai 14

adminleo