MIMBA ZA MAPEMA: Team Embrace na Inua Mama mko wapi?
Na FARHIYA HUSSEIN
MIEZI michache iliyopita, viongozi wanawake chini ya mwavuli wa Team Embrace walionekana wakiwa wamevaa nguo zinazofanana huku wakisafiri kutoka kaunti moja hadi nyingine wakiendesha kampeni za hamasisho la Wakenya kuridhia Mpango wa Maridhiano (BBI).
Wanasema wanaunga mkono maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Nalo kundi la Inua Mama ambalo linaegemea upande wa Naibu Rais William Ruto lilionekana pande mbalimbali za nchi likitangaza limejitolea kikamilifu kuwezesha jinsia ya kike.
Kivyovyote vile, makundi haya yalikuwa yakitangaza kuwa mtoto msichana na mwanamke ana mwanga wa matumaini.
Walionekana kushughulikia masilahi ya wanawake na wasichana, lakini yumkini zilikuwa ni ajenda zao za kisiasa zinazozingatia “viongozi kujizolea sifa.”
Wakati mmoja, waliweka kando tofauti zao na kuungana kwa kusukuma Mswada wa Sheria ya Jinsia bungeni.
Sasa kuna changamoto kubwa, visa vya idadi ya ujauzito miongoni mwa wasichana wa shule vikiongezeka nchini.
Huku kidole cha lawama kikielekezewa walimu na wazazi, viongozi wamekuwa kimya huku wachache wao wakionekana wakiongea wazi juu ya suala hilo.
Wawakilishi wa wanawake wanapokea kiasi fulani cha fedha za usawazishaji kutoka mfuko wa serikali kuu – NGAAF – kila mwaka wa fedha unaokusudiwa kuwasaidia kupigania na kuunga mkono maswala kama haya katika jamii zao.
Walakini, majukumu haya sasa yangekuwa yamelala lau sio mashirika ya kijamii.
Swali linabaki wako wapi wakati huu wa janga la Covid-19? Mbona hawaonekani mstari wa mbele kupigania wahasiriwa na wanawake wanaonyanyaswa kingono na wasichana wanaonajisiwa?
Mkurugenzi wa Jamii Initiatives, Bi Fatuma Juma anasema wawakilishi wa wanawake wamekuwa kimya wakati jamii inawategemea sana.
“Kujitolea kwao kutumikia jamii yahitajika kwa sana sasa. Lakini wanaonekana wakati wanahitaji msimamo wa kisiasa,” anasema Bi Juma.
Kulingana naye, mashirika ya asasi hizo za kiraia – CSOs – yameachwa peke yao kufundisha wanawake na wasichana kuhusu haki zao na umuhimu wa kutetea haki zao.
Mashirika sasa yanafanya mafunzo hayo kupitia mikutano ya Zoom.
Wiki mbili zilizopita, diwani maalum katika Bunge la Kaunti ya Mombasa, Bi Amriya Boy Juma aliwasilisha hoja ambapo aliuliza ni nini idara husika zinafanya kuhusu ujauzito kukithiri miongoni mwa vijana wa kike.
Kikao hicho cha bunge kupitia ofisi ya karani baadaye kiliandika barua kwa idara za elimu, afya na vijana kikitaka majibu ambayo bado hayajapokelewa.
Mkurugenzi wa Shirika la Lend A Voice Africa, Bi Maureen Magak anasema waliamua kuchukua hatua mikononi mwao wenyewe na kuanza kufanya kazi kushughulikia maswala yanayohusu wasichana na wanawake.
“Tulianzisha unaoegemea uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake na wasichana kupitia utengenezaji wa sabuni. Hii ni hatua ya kupunguza mzigo wa kifedha unaoletwa na umaskini ambao unasukuma baadhi ya vijana kuhadaika huko nje na baadaye kupachikwa mimba. Tumefunza wasichana 12 hadi sasa,” alisema Bi Magak.
Viongozi sasa wamehimizwa kuzindua kampeni za uhamasishaji katika kaunti zao.
“Wanapaswa kuungana mikono na wazazi na walimu na kuelewa sababu za ujauzito ambao mara nyingi huvunja ndoto za wasichana na kukandamiza hatma yao,” alisema mwanamke mwingine, Bi Patricia Peris.
Ripoti ya mwaka wa 2019 iliyoandaliwa na Baraza la Kitaifa la Idadi ya Watu na Maendeleo (NCPD) ilionyesha kuwa wasichana 20,828 ambao walikuwa na ujauzito walikuwa na umri kati ya miaka 10 na 14 wakati 349,365 walikuwa na umri wa miaka 15-19.