Manuel Pellegrini kuanza kunoa vijana wa Real Betis msimu ujao
Na CHRIS ADUNGO
KLABU ya Real Betis inayoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), imemwajiri kocha wa zamani wa West Ham United na Manchester City, Manuel Pellegrini kuwa mkufunzi wao kwa mkataba wa miaka mitatu.
Pellegrini ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Real Madrid, Villarreal na Malaga katika kipute cha La Liga, alitimuliwa na West Ham United mnamo Disemba 2019.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 66 ambaye ni mzawa wa Chile sasa atahudumu kambini mwa Betis hadi Juni 2023 baada ya kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake mwanzoni mwa msimu ujao wa 2020-21.
Akiwa Man-City alikohudumu kwa miaka mitatu, Pellegrini aliwaongoza miamba hao kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2013-14 na mataji mengine mawili ya League Cup (EFL Carabao).
“Real Betis wamejinasia huduma za kocha Pellegrini, mmoja kati ya wakufunzi wa haiba kubwa zaidi katika ulingo wa soka. Atakuwa nasi kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo na tunaamini kuwa ujio wake utafufua makali ya kikosi,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Betis.
Pellegrini anajaza nafasi ya mtangulizi wake, Joan ‘Rubi’ Francesc Ferrer ambaye alifurushwa na Betis mnamo Juni 21, 2020 baada ya kushuhudia kikosi chake kikizamishwa na Athletic Bilbao kwa bao 1-0 katika La Liga.
Mkurugenzi wa Spoti, Alexis Trujillo atadhibiti mikoba ya Betis hadi mwishoni mwa kampeni za msimu huu. Aliwahi kuchezea Betis zaidi ya mechi 200.
Rubi alitimuliwa na Betis baada ya mechi tatu pekee tangu kurejelewa kwa soka ya La Liga.