Habari

COVID-19: Visa vipya 497 vyathibitishwa idadi jumla ikifika 10,791

July 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

KENYA kufikia Jumanne imeandikisha visa 497 zaidi vya Covid-19.

Waziri Msaidizi kaika Wizara a Afya Dkt Mercy Mwangangi amesema takwimu hizo zimebainika kutoka kwa sampuli 4,922 zilizofanyiwa vipimo katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

“Kufikia sasa Kenya ina jumla ya visa 10,791 vya virusi vya corona,” Dkt Mwangangi akasema katika kikao na wanahabari Afya House, Nairobi, ambacho huandaliwa kuelezea hali ya maambukizi nchini.

Wakati huo huo, wagonjwa watano wa ugonjwa huo wamefariki, idadi hiyo ikifikisha jumla 202 walioangamizwa na virusi vya corona.

Akipongeza jitihada za wahudumu wa afya, Dkt Mwangangi ametangaza kuwa wagonjwa 70 wameruhusiwa kuondoka katika vituo mbalimbali vya afya nchini, baada ya kuthibitishwa kupona kabisa.

Idadi hiyo inafikisha jumla ya 3,017 wagonjwa waliothibitishwa kupona corona nchini Kenya.

Katika visa vya Jumanne, 480 ni Wakenya huku 17 wakiwa raia wa kigeni, wizara ya afya ikisema mgonjwa wa umri mdogo amekuwa na miaka miwili, mkubwa miaka 81.

Kaunti ya Nairobi imeandikisha visa (292), Kiambu (62), Kajiado (51), Machakos (30), Mombasa (28), Busia (10), Uasin Gishu (8), Nakuru (5) na Makueni (3).

Aidha, Meru, Narok na Nyeri, zimethibitisha wagonjwa wawili kila kaunti. Kilifi, Laikipia, Kericho, Nandi, na Kakamega, zimeandikisha kisa kimoja kila moja.

Wizara ya Afya imeendelea kuhimiza umma kutilia mkazo sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia kuenea kwa Covid-19, ugonjwa ambao sasa ni kero la kimataifa.