Michezo

Obiri, Kipruto wapata vibali vya kunogesha kivumbi cha Wanda Diamond League nchini Ufaransa

July 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa dunia katika mbio za mita 5,000 kwa upande wa wanawake, Hellen Onsando Obiri na mfalme wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Conseslus Kipruto watanogesha kivumbi cha Wanda Diamond League mnamo Agosti 14, 2020 jijini Monaco, Ufaransa.

Wawili hao wamekuwa wa kwanza kupata vibali na pasipoti za Schengen zinazowakubalia kuingia katika mataifa mbalimbali ya Muungano wa Bara Ulaya (EU) kwa minajili ya kushiriki mashindano mbalimbali yatakayoandaliwa kuanzia mwezi ujao.

Obiri ambaye pia ni bingwa wa Jumuiya ya Madola na malkia wa Afrika katika mbio za mita 5,000 atapania kutumia mbio hizo kuandikisha muda bora zaidi kuliko ule wa dakika 14:26.72 aliotumia kujinyakulia nishani ya dhahabu katika Riadha za Dunia za 2019 jijini Doha, Qatar.

Atakabiliana na ushindani mkali kutoka kwa mwanariadha matata mzawa wa Ethiopia na raia wa Uholanzi, Sifan Hassan aliyetawala mbio za mita 10,000 katika Riadha za Dunia mwaka jana kwa muda wa dakika 30:17.62

Hassan, 27, alijishindia pia dhahabu katika mbio za mita 1,500 jijini Doha kwa muda wa dakika 3:51.95 na kuweka rekodi ya kuwa mtimkaji wa kwanza kuwahi kutamalaki fani za mbio hizo katika makala moja ya Riadha za Dunia.

Kwa upande wake, Kipruto ambaye pia ni bingwa wa Olimpiki, atalenga kuendeleza babe uliomzolea medali ya dhahabu mwaka jana nchini Qatar baada ya muda wa dakika 8:01.35

Bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot, mfalme wa Jumuiya ya Madola Elijah Manangoi, Timothy Sein, Winny Chebet na Vincent Keter wanaonolewa kwa sasa na kocha Bernard Ouma, ni miongoni mwa Wakenya wengine wanaotazamiwa kupata vibali vya kunogesha duru ijayo ya Damond League nchini Ufaransa.