Pamzo mwingi wa imani atahifadhi kikosini wanasoka sita ambao mikataba yao imetamatika
Na CHRIS ADUNGO
KIKOSI cha Posta Rangers cha kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo kipo katika hatari ya kupoteza huduma za wanasoka sita ambao bado wanasubiri kandarasi mpya baada ya zile za awali kukamilika mnamo Juni 30, 2020.
Hata hivyo, Pamzo ambaye amekataa kufichua majina ya sita hao kwa hofu kwamba wataanza kunyemelewa na wapinzani wao, amesisitiza kuwa masogora hao wangalipo katika mipango yake ya baadaye kikosini.
Mkufunzi huyo wa zamani wa Tusker sasa ametaka usimamizi wa Posta kufanya hima na kurefusha mikataba ya wanasoka hao japo wawili kati ya sita hao wameanza kuhemewa na vikosi vya nje ya nchi.
Pamzo ambaye ni beki wa zamani wa Harambee Stars ameshikilia kuwa wanasoka hao ni miongoni mwa waliomridhisha pakubwa katika kampeni za Rangers msimu huu na kubwa zaidi katika matamanio yake ni kuendelea kujivunia huduma zao.
“Kandarasi za wachezaji sita wa Rangers zilitamatika mwishoni mwa Juni na nimeanzisha mazungumzo na klabu ili kuhakikisha kuwa zinarefushwa. Hawa ni wanasoka chipukizi ambao bado nitawahitaji kuchangia ushindani mkali kikosini,” akasema Pamzo ambaye pia aliwahi kudhibiti mikoba ya wanabenki wa KCB.
Mbali na kufukuzia saini za wanasoka hao sita, Pamzo pia amefichua kwamba wapo chipukizi wengi ambao wamekuwa wakibisha milango ya Rangers kwa nia ya kuingia katika sajili rasmi ya kikosi hicho.
“Makocha wengi hukosa usingizi wakati ambapo mikataba ya wanasoka wao tegemeo hukatika. Huku nikisalia na tumaini kwamba hakuna mchezaji yeyote ambaye ataagana nasi muhula huu, naaminishwa zaidi na idadi kubwa ya chipukizi ambao wanakamia fursa za kuvalia jezi za Rangers,” akasema Pamzo ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya soka.
Pamzo pia ameendelea kurai serikali kupitia Wizara ya Michezo kuwapa msaada baadhi ya wanasoka ambao wameathiriwa vibaya zaidi kutokana na janga la corona.
Rangers ni miongoni mwa klabu sita za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ambazo hazikushirikishwa kwenye mradi wa serikali ambao umeshuhudia wanasoka wa klabu 12 za ligi kuu zilizoathiriwa zaidi na corona wakipokezwa malipo ya Sh10,000 kila mwezi.