Changamoto kutokana na janga la corona zayumbisha wachezaji wa Ukunda Vision Starlets FC
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
SOKA ya wanawake inaendelea kunawiri huku wasichana wengi wakipendelea kujiunga na klabu za mchezo huo wakiwa na sababu mbalimbali na hasa zile za kutaka watambulike na kupata umaarufu.
Soka ya wanawake inathaminiwa zaidi katika kaunti nne kati ya sita za eneo la Pwani ambapo kumekuwa kunaundwa klabu kadhaa huku waanzilishi wake wakitoa sababu za maamuzi yao ya kuunda klabu hizo.
Kaunti ambazo zina klabu nyingi za soka ya wanawake ni Mombasa, Kilifi, Taita Taveta na Kwale.
Mojawapo ya klabu zenye wachezaji wengi zaidi ni ile ya Ukunda Vision Starlets FC ambayo ilieleza changamoto inayowafika wasichana wanaoichezea; vikosi vitatu vya timu hiyo.
Katika mahojiano na baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo ya Ukunda, Kaunti ya Kwale, walisema janga la corona limewakuta wakiwa wanajiandaa kushiriki kwenye Michezo ya Shule ambayo yanafanyika kutoka ngazi za mashinani za kaunti ndogo hadi za kitaifa.
Wachezaji hao, wengi wao wakiwa wanafunzi wa shule za sekondari wameeleza changamoto wanazopata wakiwa majumbani kwa kipindi hiki cha Covid-19 huku wakidai kimeathiri pakubwa juhudi zao za kuendeleza vipaji vya uchezaji wao.
“Nilijitayarisha vilivyo kuhakikisha naiwakilisha shule yangu vizuri tupate kufika mbali kwenye michezo ya shule lakini janga la corona lilipozuka, nilikata tamaa nikaona ndio mwisho wa juhudi zangu za kuimarisha hali ya uchezaji wangu,” alisema, Jackline Sanga.
Jackline, mwanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya Mkwakwani anayechezea nafasi ya ulinzi, anasema anasikitika kuwa janga hilo limemrudisha nyuma katika kuendeleza kipaji chake sababu amepoteza muda mrefu bila ya kufanya mazoezi.
Mwanafunzi mwingine wa kidato cha nne wa shule ya Mwanambeyu, Ruth Kadzo anasema tangu janga la corona lianze na kwa kipindi chote hicho, amekuwa akihuzunika kufikiria kuwa ndoto yake ya kuwa mchezaji mwenye jina kubwa imetokomea.
“Nimekuwa na huzuni kubwa kwanza kukosa masomo pamoja na kuiwakilisha shule yangu kwenye michezo ya shule na pia kukosa kuwa na wenzangu wa Ukunda Vision Starlets. Hakika ningali nina masikitiko na yataondoka tu pale tukianza kucheza mpira,” akasema mchezaji huyo wa safu ya ushambulizi.
Mwanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya Leisure Rondwe, Mgeni Hassan, anasema amekosa furaha kutokana na ukosefu wa kufanya mazoezi pamoja na wenzake shuleni na timu yake ya Ukunda Vision.
“Nimekuwa na furaha nikicheza na wenzangu lakini kwa kipindi chote hiki, nimekuwa nikikaa nyumbani bila ya kufanya mazoezi nikiogopa kuambukizwa corona,” akasema Mgeni.
Mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa shule ya Lukore Secondary, Elizabeth Dama, amesema ameathirika kisaikolojia tangu janga la corona litangazwe.
“Kukosa kucheza mpira na kuwa karibu na wenzangu kunanifanya nihuzunike wakati mwingi,” akasema Elizabeth.
Kocha wa timu hiyo, Elvina Baya amesema kuwa kuanzia sasa, atawapangia programu kupitia kwa mtandao wa WhatsApp kuhakikisha wanaanza mazoezi kwani amewaona kuwa changamoto kubwa yao ni kukosa kuwa pamoja na kucheza mpira.
Elvina alisema atashirikiana na Mkurugenzi wa Ufundi, Martin Wekesa kuhakikisha wanawasiliana na wazazi wa wachezaji wao kwa kuwatumia jinsi watoto wao watakavyofanya mazoezi.
“Tutaanza kuwasiliana na wachezaji wetu wote kuwafahamisha waanze kujitayarisha kwani mara serikali itakaporuhusu wanamichezo warudi viwanjani, wawe wako katika hali nzuri,” akasema mkufunzi huyo aliyeeleza imani kuwa timu yao itafanya vizuri ligi itakapoanza.
Daktari David Sila wa hospitali ya Beach Road Medical Clinic amesema wasichana wa timu hiyo watakapoanza kwenda uwanjani kufanya mazoezi, atafika huko kuwapa mawaidha madhara ya kuwa pamoja bila ya kupata ushauri kutoka kwa maofisa wa afya.
“Nitafika uwanjani kuwafahamisha madhara ya wachezaji kutangamana bila ya ushauri wa wataalamu kuhusu kujitakasa mikono kwa kutumia sabuni na kuweka nafasi baina yao,” akasema Daktari Sila.
Timu hiyo ya Ukunda Vision Starlets ilishiriki kwenye Ligi ya FKF Pwani kusini ambapo ilifanikiwa kufika fainali.
“Tumeomba FKF itupandishe hadi Ligi ya Taifa ya soka ya Wanawake kwani tunaweza na hata tulishindwa kwa bahati mbaya kwenye mechi ya fainali,” akasema.