WASONGA: Magoha afafanue kuhusu masomo ya ziada mitaani
Na CHARLES WASONGA
WAZAZI wanafaa kuchukua tahadhari kubwa baada ya serikali kuruhusu walimu kuendesha masomo ya ziada mitaani na vijijini licha ya kuwepo kwa sheria inayoharamisha mafunzo kama hayo.
Sehemu ya 37 ya Sheria ya Elimu ya Msingi inaharamisha masomo ya ziada nyakati za likizo.
Lakini majuzi Waziri wa Elimu, George Magoha alisema kuwa walimu wanaweza “kuelewana” na wazazi ili wakodi vyumba mitaani na vijijini ambako wanafunzi watasomeshwa.
Hii ni baada yake kutangaza kuwa shule zitasalia kufungwa hadi Januari 2021, baada ya kubainika kuwa wizara yake haijaweka imikakati ifaayo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona shuleni.
Ndiposa ni sharti wazazi wawe waangalifu ili watoto wao wasije wakatumbukia katika hatari ya kudhulumiwa na hata kuambukizwa virusi vya corona wakati wa mafunzo haya ya ziada.
Hii ni kwa sababu Waziri Magoha aliruhusu masomo ya ziada pasina kutoa mwongozo kamili utakaozingatiwa na wahusika wakati wa mafunzo hayo.
Kile Profesa Magoha alisema ni kwamba walimu wanafaa kuhakikisha kuwa masharti yote ya kuzuia kuenea kwa virusi vya Covid-19 yanazingatiwa wakati wa mafunzo, na kwamba walimu hawafai kutoa ada zozote.
Lakini hakubainisha ni nani atagharamia ada za kukodisha kumbi au majumba ambako wanafunzi watafundishwa katika mitaa ya miji na vijijini.
Matapeli
Pia hakuna mikakati yoyote ambayo wizara yake imeweka kuhakikisha watu fulani walaghai hawatatumia nafasi hii kujifanya ni walimu ilhali lengo lao ni kuwapunja wazazi au kuwadhulumu watoto kimwili.
Dhihirisho la hofu hii ni kuwa siku chache baada ya Profesa Magoha kutangaza kulegezwa kwa marufuku ya masomo ya ziada, vijikaratasi vimeanza kubandikwa katika mitaa kadha ya Nairobi watu wanaodai ni walimu wakitangaza huduma hizo kwa malipo.
Pia hakuna utaratibu wowote ambao umewekwa na serikali kuwakagua watu kama hawa ili kubaini ikiwa ni walimu waliosajiliwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) au ni matapeli.
Hii ni hatari zaidi wakati kama huu ambapo visa vya watoto wasichana kunyanyaswa kingono na kupachikwa mimba vimekithiri mno.
Isitoshe, Waziri Magoha hakufafanua iwapo wizara yake na ile ya Afya zitatuma maafisa kukagua kumbi ambako watoto watakuwa wakifunzwa kuhakikisha, kwa mfano, zina nafasi tosha za kuzuia msongamano.
Swali ni je, ikiwa serikali imeweka kanuni za kuzingatiwa katika sehemu za ibada na katika sekta ya uchukuzi mbona isifanye hivyo kwa mafunzo ya ziada?
Mafunzo haya yanaweza kuwa ya manufaa makubwa zaidi kwa wanafunzi na wazazi ikiwa Wizara ya Elimu itatoa mwongozo mahsusi wa kuzingatiwa.
Ilivyo sasa ni kwamba itakuwa vigumu kwa walimu kuendesha mafunzo hayo bila kutoza malipo na katika mazingira salama kwa wanafunzi.
Kwa hivyo, wazazi watahadhari kabla ya kuwasajili watoto wa mafunzo kama haya.