Harry Kane apitisha idadi ya mabao 200 akicheza soka katika kiwango cha klabu
Na CHRIS ADUNGO
MSHAMBULIAJI Harry Kane alifikisha zaidi ya mabao 200 katika taaluma yake ya usogora kwenye ngazi ya klabu baada ya kutikisa wavu mara moja na kusaidia Tottenham Hotspur kuwapepeta Newcastle United 3-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Julai 15, 2020.
Matokeo hayo yaliweka hai matumaini ya Tottenham ya kushiriki soka ya bara Ulaya (Europa League) msimu ujao wa 2020-21. Hii ni baada ya masogora hao wa kocha Jose Mourinho kupaa hadi nafasi ya saba kwa alama 55 kwenye msimamo wa jedwali la EPL.
Ilikuwa mara ya kwanza baada ya majaribio manane kwa Mourinho kuongoza kikosi chake kusajili ushindi katika kipute cha EPL uwanjani St James’ Park.
Licha ya wenyeji kuanza mechi kwa matao ya juu, Tottenham waliojiweka kifua mbele kunako dakika ya 27 kupitia bao la fowadi Son Heung-Min.
Nusura Dwight Gayle asawazishe mambo mwishoni mwa kipindi cha kwanza ila kombora lake likabusu mwamba wa goli la Tottenham ambao mwishowe walitepetea na kumruhusu Matt Ritchie kufanya mambo kuwa 1-1 kunako dakika ya 56.
Ingawa bao hilo lilitarajiwa kurejesha Newcastle mchezoni, Tottenham walihisi kuamshiwa hasira na wakafunga la pili kunako dakika ya 60 kupitia kwa Kane aliyeshirikiana vilivyo na Steven Bergwijn aliyetokea benchi.
Bao hilo lilikuwa la 200 kwa Kane kufunga kutokana na mechi 350 akivalia jezi za klabu mbalimbali. Kati ya mabao hayo, 184 yametokana na mechi ambazo amewachezea Tottenham huku mengine 16 yakitokana na michuano ambayo amechezea klabu za Millwall, Leyton Orient na Leicester City.
Nahodha huyo wa Tottenham na timu ya taifa ya Uingereza, alipachika wavuni bao lake la 201 mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Martin Dubravka kutokana na fataki ya Erik Lamela.
Tottenham kwa sasa wanajiandaa kuwaalika Leicester City kwa gozi kali la kufa kupona katika EPL mnamo Julai 18 kabla ya kufunga rasmi kampeni za msimu huu dhidi ya Crystal Palace mnamo Julai 26 uwanjani Selhurst Park.
Kwa upande wao, Newcastle wamepangiwa kupepetana na Brighton na Liverpool kwa usanjari huo katika mechi zao za mwisho msimu huu.