• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
Yaamuliwa mechi 4 kuchezwa kwa siku moja katika Kombe la Dunia 2022

Yaamuliwa mechi 4 kuchezwa kwa siku moja katika Kombe la Dunia 2022

Na CHRIS ADUNGO

JUMLA ya mechi nne zitasakatwa kila siku katika hatua ya makundi wakati wa fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Qatar mnamo Novemba – Disemba 2022.

Haya ni kwa mujibu wa Shirikisho la Duniani (Fifa) ambalo limefichua kwamba mechi zote za makundi zitapigwa katika kipindi cha siku 12.

Aidha, hakuna ratiba itakayotolewa kuonyesha kwamba mechi fulani zitachezewa katika viwanja fulani mahsusi hadi wakati droo ya mwisho ya fainali hizo itakapotolewa mnamo Machi 2022.

Mechi zote za raundi mbili za kwanza zitachezwa kila siku kuanzia saa saba mchana, saa kumi alasiri, saa moja jioni na saa nne usiku katika viwanja vinane tofauti.

Kwa kuwa viwanja vikuu vya Qatar havijatengana sana, ina maana kwamba mashabiki na wanahabari watakuwa na uwezo wa kuhudhuria jumla ya angalau mechi mbili siku moja.

Kwa mechi zote, isipokuwa tatu, patakuwepo na kipindi cha siku tatu za mapumziko.

Hapakuwepo na haja ya vikosi, mashabiki na wanahabari kutumia ndege au kujipata katika ulazima wa kufunga safari ndefu za treni au magari kuhudhuria mechi inayofuata baada ya nyingine kukamilika.

Mechi zote za mwisho za makundi zitachezewa katika wakati mmoja ambapo zile za raundi ya kwanza zitaanza saa kumi na mbili jioni na za raundi ya pili kunogeshwa saa nne usiku.

Mechi ya ufunguzi katika fainali hizo, ambayo itawashirikisha wenyeji Qatar, itachezewa katika uwanja wa Al Bayt viungani mwa mji wa Al Khor mnamo Jumatatu ya Novemba 21. Uwanja huo una uwezo wa kubeba hadi mashabiki 60,000 walioketi.

Fainali itatandaziwa katika uwanja wa Lusail jijini Doha mnamo Jumapili ya Disemba 18, 2022. Uga huo una uwezo wa kubeba hadi mashabiki 80,000 walioketi.

Tarehe ya kuanza kwa mchujo wa kufuzu kwa fainali hizo miongoni mwa mataifa ya bara Ulaya bado haijatolewa japo droo ya mechi hizo za kufuzu inatarajiwa kutolewa wakati wowote kuanzia Disemba 1, 2020.

You can share this post!

Ojaamong akana kwenda Ujerumani kuponda raha

Kamishna awaonya wanasiasa wanaotaka kuchafua Kazi Mtaani

adminleo