Habari

Kilichoanza kama pepezi sasa ni upepo wa uharibifu Mtwapa

July 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

FAMILIA tatu katika Kaunti ya Kilifi zimeachwa bila makao baada ya upepo mkali kung’oa mapaa ya nyumba zao usiku wa kuamkia leo Ijumaa.

Nyumba zilizoathirika ni za eneo la Vingazini, Mtwapa.

Kulingana na aliyeshudia tukio hilo, Bi Tatu Jumwa, alisema walisikia kelele mwendo wa saa moja usiku kutoka kwa majirani wao.

Bi Jumwa alieleza kuwa walipotoka nje kushuhudiwa kilichokuwa kinaendelea, waliona paa la nyumba ya jirani yao likiwa limevunjika.

Alisema kuwa hakuna aliyejeruhiwa katika mkasa huo.

“Nyumba moja kati ya zilizoharibiwa ni jirani na yangu. Iko mara mbili; sehemu ya mbele inakaliwa na baba na vijana wawili na sehemu ya nyuma iko na familia ya watoto saba na wazazi wao,” akasema.

 

Makazi yaliyoharibiwa na upepo unaovuma eneo la Mtwapa, Kilifi katika hii picha ya Julai 17, 2020. Picha/ Mishi Gongo

Familia hizo sasa zinaomba msaada kutoka kwa wenye uwezo walio na moyo wa kusaidia.

Mmoja wa wahasiriwa Bw Henry Chengo alisema japo hakuna aliyejeruhiwa katika mkasa huo, maisha yao yameathirika kwani hawana sehemu nyingine ya kuhamia.

“Tunaomba msaada kutoka kwa wenye moyo wa kusaidia kuturekebishia paa hili. Jinsi muonavyo paa lililokuwa ni hafifu na sasa tunataka paa madhubuti ambalo litavumilia upepo mkali ambao unaendelea kushuhudiwa,” akasema.

Siku ya Alhamisi idara ya utabiri wa hali ya hewa ilitoa tahadhari ya kuwepo kwa upepo mkali na mawimbi makali katika kaunti za Marsabit, Turkana, Samburu, Mandera, Wajir, Isiolo, Garissa, Kitui, Makueni, Taita Taveta, Tana River, Lamu, Kilifi, Mombasa, na Kwale.

Katika tangazo walilotuma katika ukurasa wao, wakuu wa idara hiyo walisema kuwa upepo huo ungevuma kuanzia mwendo wa adhuhuri.

Wakawaonya wakazi kuwa upepo huo unaweza kung’oa mapaa ya nyumba, miti na kuharibu majengo.

Aidha waliwaonya kuwa mawimbi makali katika fuo za Bahari Hindi yanaweza kufanya madau kuzama na kutatiza kuona hivyo kuhatarisha maisha ya wavuvi na wanaoshiriki katika michezo ya baharini.