Kadinali Njue ataka Wakristo watumie fursa iliyopo kuomba Mungu amalize Covid-19
Na BENSON MATHEKA
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki nchini Kadinali John Njue, Jumapili amewahimiza Wakristo kutumia kufunguliwa kwa makanisa kuomba Mungu amalize janga la corona.
Akiongoza misa ya kwanza mbele ya waumini baada ya miezi mitatu katika Kanisa la Holy Family Basilica jijini Nairobi, Kadinali Njue amewaambia Wakristo kuwa viongozi wa makanisa waliwakosa sana katika muda maeneo ya ibada yalipokuwa yamefungwa.
“Imekuwa zaidi ya miezi mitatu ambayo hatukuweza kukutana kwa ibada hata siku za Jumapili kama hii kwa sababu ambazo kila mtu anafahamu. Lakini tunashukuru Mungu, kwamba tumeweza kuwa na ibada ana kwa ana kama hii. Tunawakaribisha kwa misa hii, tunatambua na tunajua ni baraka,” akawaambia waumini wasiozidi mia moja waliohudhuria misa.
Amewataka maaskofu na mapadre wa Kanisa Katoliki kuzingatia kanuni za Wizara ya Afya za kuzuia msambao wa virusi vya corona.
“Leo tunafungua tena ibada zetu makanisani na tunashukuru Mungu kwa kutupatia fursa hii. Wakristo wengi wamekuwa na hamu ya kukutana kwa ibada na tunashukuru Mungu amekutanisha kondoo wake tena,” alisema.
Mnamo Julai 6, 2020, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza maeneo ya ibada kufunguliwa kwa awamu kufuatia mwongozo uliotayarishwa na baraza la viongozi wa Kidini.
Ingawa baadhi ya makanisa yaliamua kutofungua yakisema masharti yaliyowekwa na baraza hilo hasa idadi ya waumini na muda wa ibada hautoshi, Kanisa Katoliki liliamua kuanza ibada.
Hata hivyo baadhi ya maaskofu wa Kanisa hilo waliahirisha kufungua hadi waandae makanisa yao kutimiza mwongozo na kanuni za wizara ya afya.