Shughuli za ujenzi wa uwanja wa kisasa Mombasa zashika kasi
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
SASA ni kazi kwenda katika uwanja wa kisasa wa Mombasa ambako kumeanza kuonekana shughuli za kutia hamu.
Kuanza kwa kazi ya ujenzi wa uwanja huo kutapunguza vilio vya mashabiki wa soka wa Mombasa na eneo zima la Pwani kwa ujumla kwani dalili njema ya kutimia kwa mradi wa ujenzi wa uwanja, imeanza kuonekana.
Harakati zinazoendelea zinawapa mashabiki matumaini sasa uwanja huo unajengwa kweli.
Katika kila sehemu ya uwanja huo, wafanyakazi, matingatinga na malori yako yakitekeleza shughuli mbalimbali za kuhakikisha wanakamilisha kazi za ujenzi wa uwanja huo wa kisasa unaosubiriwa kwa ham una wapenzi wa mpira wa miguu.
Afisa Mkuu wa Michezo wa Serikali ya Kaunti ya Mombasa, Innocent Mugabe amewapa tamaa wapenzi wa mchezo huo kuwa baada ya mwaka mmoja na miezi sita, wataweza kufanikiwa kushuhudia mechi kubwa zikiwemo za kimataifa.
“Ni kazi tu katika uwanja wa kisasa wa Mombasa na nina imani kubwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu, uwanja huo utaweza kukamilika kujengwa na kuanza kutumika kwa mechi za kitaifa na kimataifa,” akasema Mugabe.
Afisa huyo amesema anaamini kwa jinsi kazi inavyoendelea uwanjani hapo, mashabiki wa soka wameanza kuwa na matumaini ya uwanja huo kukamilika kwa kipindi alichosema.
“Nina furaha kuona harakati za ujenzi zinavyoendelea katika uwanja wetu huo na sasa nina matumaini makubwa utaweza kukamilika. Tunatamani kushuhudia mechi kubwa ambazi tumezikosa kwa kipindi cha miaka mingi,” amesema aliyekuwa Meneja wa Feisal FC, Abdillahi Bashasha.
Bashasha aliyekuwako uwanjani hapo anasema amevutiwa mno kuwaona wafanyakazi wakishughulikia ujenzi wa sehemu za uwanja huo na hali ilivyo uwanjani wakati huu, kunampa moyo mkubwa kuwa sasa “Stadium ya Mombasa is a reality.”
Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Cosmos FC, Aref Baghazally amesema kuwa juhudi zinazofanywa na serikali ya kaunti hiyo ya kujenga Stadium ya Mombasa zinastahili kusifiwa sababu hivi sasa ndipo kazi inafanyika.
“Ninafurahikia na jinsi kazi ya ujenzi inavyofanyika kwani inatupa moyo kuwa uwanja huo utakamilika kwa wakati mzuri. Hakika tulikuwa na wasiwasi kwa kuwa kulikuwa na watu wachache na harakati zilikuwa ndogo, lakini sasa yapigwa kazi muruwa,” akasema Baghazally.
Kati ya shughuli zilizokuwa zikiendelea siku ya Jumamosi ni pamoja na kukata vyuma na kuviweka sehemu zinazohitajika, kukusanywa kwa mchanga na simiti kutengeneza mawe na kukata miti, ukiwemo mti wa mwembe ambao ulipandwa mwaka 1945, miaka 75 iliyopita.
Uwanja huo ulikuwa maarufu miaka ya kale ambapo timu zilizokuwa zikitamba jimbo la Pwani, Liverpool na Feisal ndizo zilizokuwa zikivutia mashabiki wengi zaidi na ndizo zilizokuwa watani wa jadi.
Nyakati hizo, uwanja hupo ulikuwa pia ukitumika kwa mechi zilizohusisha klabu hizo za Liverpool (Mwenge) na Feisal kucheza mechi za kirafiki dhidi ya timu maarufu za jijini Dar es Salaam za Sunderland (sasa Simba) na Young Africans (Yanga).
Mbali na kualika timu hizo za Tanzania, timu hizo za kale ziliwahi kucheza mechi na klabu za India, Uganda na Mwenge kuwahi kucheza na timu ya Norwich ya Uingereza ambayo ilikuwa ikishiriki Ligi Kuu ya England.
Stadium ya Mombasa mara kadhaa ulitumika kwa mechi za Kombe la Gossage ambalo lilipiganiwa na nchi za Tanganyika (Tanzania Bara), Zanzibar, Uganda na Kenya Pia iliwahi kuandaa mechi muhimu ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki kati ya Yanga na Luo Union.