Serikali yajiandaa kwa hatua mpya kukabili corona
Na DIANA MUTHEU
SERIKALI imeanza kujiandaa kutoa kanuni mpya zitakazofuatwa kupambana na virusi vya corona ambavyo vinaendelea kusambaa kwa kasi kitaifa.
Rais Uhuru Kenyatta Jumatatu alitangaza kikao maalum kati ya serikali kuu na zile za kaunti mnamo Julai 24, ambapo inatarajiwa watakubaliana kuhusu kanuni mpya ziazohitajika.
Kupitia taarifa kutoka kwa msemaji wa Ikulu, Bi Kanze Dena, Rais Kenyatta alithibitisha tayari kaunti 44 zina wagonjwa wa Covid-19 huku idadi ikitarajiwa kufika upeo kati ya Agosti na Septemba.
“Tutaangazia jinsi ugonjwa huu unavyobadilika, na ni vipi unaweza kujitokeza katika mwezi wa Agosti na Septemba humu nchini,” ikasema taarifa hiyo.
Jana, Naibu Waziri wa Afya, Dkt Rashid Aman alitangaza watu 418 kuambukizwa, wakafikisha idadi ya jumla hadi 13,771.
Mtangazaji maarufu wa habari, Bw Jeff Koinange, alithibitisha kwamba yeye ni mmoja wa waliopatikana na virusi hivyo.
“Niko salama, sionyeshi dalili zozote na familia yangu pia iko salama. Watu wote niliotagusana nao wamefahamishwa. Kwa sasa nimejitenga kutoka kwa jamii,” akasema.
Jana, watu wanne walitangazwa kufariki na kufikisha idadi jumla kuwa 238.
Akitoa matangazo hayo akiwa katika makao makuu ya wizara jijini Nairobi, Dkt Aman alisema wagonjwa 494 nao waliruhusiwa kuondoka hospitalini, hiyo ikifikisha idadi ya waliopona kuwa 5,616.
Miongoni mwa waliopona 465 walikuwa wanahudumiwa nyumbani huku 29 wakiwa hospitalini.
“Mgonjwa mdogo zaidi ni mtoto wa mwaka mmoja na mkubwa zaidi ana miaka 86,” akasema Dkt Aman.