Mastaa wa zamani wa EPL waipa Basaksehir ubingwa wa ligi
Na CHRIS ADUNGO
ISTANBUL Basaksehir walijitwalia ubingwa wa kwanza la Ligi Kuu ya Uturuki (Turkish Super Lig) mnamo Julai 19, 2020 baada ya kuwapokeza Kayserispor 1-0.
Bao hilo la ushindi kupitia kwa fowadi Mahmut Tekdemir liliwazolea Basaksehir taji la kwanza katika historia yao ya kushiriki soka ya haiba kubwa.
Mvamizi wa zamani wa Chelsea, Demba Ba, aliyekuwa beki wa Liverpool Martin Skrtel na difenda wa zamani wa Man-City na Arsenal, Gael Clichy walikuwa sehemu ya kikosi cha Basaksehir kilichojinyanyulia ufalme wa Turkish Super Lig ikisalia mechi moja zaidi kwa soka ya kampeni za msimu huu kutamatika rasmi.
Hadi walipotwaa ubingwa, Basaksehir walikuwa wameambulia nafasi ya pili kwenye Turkish Lig katika kipindi cha misimu miwili mfululizo.
Waliongoza jedwali katika kampeni za msimu uliopita wa 2018-19 kabla ya utepetevu wao katika mechi nne za mwisho kuwaponza na hatimaye kuambulia nafasi ya pili nyuma ya Galatasaray waliotoka nyuma na kuwazidi kwa pointi mbili zaidi.
Iwapo Basaksehir na Manchester United watasonga mbele kwenye hatua ya 16-bora ya Europa League msimu huu, basi vikosi hivyo viwili vitakutana kwenye robo-fainali ya kivumbi hicho nchini Ujerumani mnamo Agosti 2020.
Basaksehir ilianzishwa mnamo 1990 ikiwa klabu ya mtaa kabla ya umiliki wake kutwaliwa na wafanyabiashara maarufu waliokuwa wandani wa karibu wa Rais Recep Tayyip Erdogan. Kati ya wanasoka walioongoza ufufuo wa makali ya Basaksehir katika kipindi cha miaka saba iliyopita ni fowadi wa zamani wa Brazil, Robinho.
Miamba wa soka ya Uturuki, Galatasaray, sasa hawatakuwa sehemu ya vikosi vitakavyonogesha soka ya bara Ulaya msimu ujao baada ya kukamilisha kampeni za Turkish Super Lig msimu huu nje ya mduara wa nne-bora. Fernerbahce wana uhakika wa kukamilisha kampeni za msimu huu katika nafasi ya saba huku Besiktas wakiwa na uhakika wa kunogesha kipute cha Europa League muhula ujao.