Michezo

Dortmund yamsajili Jude Bellingham

July 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

UHAMISHO wa kiungo chipukizi wa Birmingham City, Jude Bellingham hadi kambini mwa Borussia Dortmund ya Ujerumani umekamilika na umerasimishwa kwa kima cha Sh4.2 bilioni.

Tineja huyo mwenye umri wa miaka 17 alisafiri Ujerumani mnamo Julai 17 kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kurejea Uingereza kwa minajili ya mchuano wa mwisho wa Birmingham dhidi ya Deepdale katika Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship).

Dortmund ambao ni washiriki wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), walilazimika kuwapiga kumbo wapinzani kadhaa wakiwemo Manchester United ili kujinasia huduma za Bellingham.

Man-United waliwahi hata kumtuma kocha wao wa zamani Sir Alex Ferguson hadi uwanjani Deepdale kumtazama Bellingham akitandaza mpira uwanjani kabla ya kuwasilishia Birmingham ombi rasmi la kumsajili kiungo huyo muhula huu.

Ingawa hivyo, mafanikio ya hivi karibuni ya Dortmund katika kuwanoa vilivyo chipukizi Jadon Sancho, Christian Pulisic na Erling Braut Haaland, yalimchochea zaidi Bellingham kuingia katika sajili rasmi ya kikosi hicho cha Bundesliga ambacho pia kimekuwa na uhakika wa kushiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Mnamo Agosti 2019, Bellingham alivunja rekodi ya mvamizi wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Trevor Francis kwa kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuwajibishwa katika kikosi cha kwanza cha Birmingham akiwa na umri wa miaka 16 na siku 38 pekee.