Michezo

Leganes, Espanyol na Maloorca watemwa La Liga

July 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA wapya wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Real Madrid waliambulia sare ya 2-2 dhidi ya Leganes katika mchuano wao wa mwisho wa msimu huu.

Sare tasa iliyosajiliwa na Celta Vigo dhidi ya Espanyol ilitosha kuwadumisha katika kampeni za La Liga muhula ujao na kuwaweka Leganes katika ulazima wa kuteremshwa ngazi.

Nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos alipachika wavuni bao lake la 12 msimu huu baada ya kukamilisha krosi ya Isco kunako dakika ya tisa. Goli la pili la masogora hao wa kocha Zinedine Zidane lilijazwa kimiani na kiungo Marco Asensio katika dakika ya 52.

Celta waliokamilisha kampeni za muhula huu katika nafasi ya 17 kwa alama 37, walifungiwa mabao yao kupitia kwa Bryan Gil na Roger Assale kunako dakika za 45 na 78 mtawalia.

Zaidi ya Leganes na Espanyo, kikosi kingine kilichoshushwa daraja kwenye kampeni za La Liga msimu huu ni Mallorca kilichomaliza katika nafasi ya 19 kwa alama 33 baada ya kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya Osasuna mnamo Julai 19, 2020.

Real kwa sasa wanajiandaa kurudiana na Manchester City katika hatua ya 16-bora ya soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ambapo watakuwa na kibarua kigumu cha kubatilisha matokeo ya 2-1 yaliyosajiliwa na Man-City dhidi yao mnamo Februari 2020.