Michezo

Mbio za Kip Keino Classic zanukia

July 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

WAANDALIZI wa mbio za Kip Keino Classic zitakazofanyika jijini Nairobi mnamo Septemba 26 wamesema wanajitahidi kadri ya uwezo kukamilisha shughuli za kuweka sawa uwanja wa Nyayo kwa minajili ya kivumbi hicho.

Kip Keino Classic ni miongoni mwa duru za kivumbi cha World Athletics Continental Tour kitakachofunguliwa rasmi jijini Turku, Finland mnamo Agosti 11, 2020.

Kipute cha Turku kimepewa jina Paavo Nurmi kwa heshima ya aliyekuwa mwanariadha nguli wa taifa hilo, Nurmi ambaye alijinyakulia medali tisa za dhahabu na tatu za fedha katika fani mbalimbali za Olimpiki zilizoandaliwa 1920 (Antwerp, Ubelgiji), 1924 (Paris, Ufaransa) na 1928 (Amsterdam, Uholanzi).

Kwa mujibu wa Barnaba Korir ambaye ni Mkurugenzi wa Duruy a Kip Keino Classic, maafisa wa kiufundi wameteua mbio hizo kuandaliwa uwanjani Nyayo kwa kuwa ule wa MISC Kasarani umetengwa na Serikali kuwa sehemu ya dharura ya kuwaweka wagonjwa wa Covid-19 iwapo idadi ya maambukizi itazidi kuongezeka na kulemea asasi zilizopo za afya.

“Maandalizi yamefikia hatua muhimu (asilimia 90) na tumekuwa na vikao kadhaa ambavyo vimezalisha matunda. Kufikia sasa, shughuli za maandalizi katika uwanja wa Nyayo zinaelekea kufikia hatua za mwishomwisho,” akasema Korir kwa kusisitiza kwamba duru ya Turku itawapa mwao zaidi kuhusu yale yanayohitajiwa kufanywa na Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) ili kufanikisha duru ya Kip Keino Classic.

Aidha, alishikilia kuwa mbio hizo za Septemba 26 zitawapa jukwaa mwafaka zaidi za kuandaa Mbio za Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 jijini Nairobi mwaka ujao.

Mbio za Continental Tour zitashirikisha nyingi za fani ambazo zimeondolewa kwenye kivumbi cha Diamond League msimu huu wa 2020 zikiwemo mbio za mita 200 na mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

Makala ya kwanza ya Continental Tour yalikuwa yafanyike humu nchini mnamo Mei 2, 2020 ila yakaahirishwa kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Licha ya duru nzima kuitwa Kip Keino Classic kwa heshima ya mwanariadha veterani Kipchoge Keino, kivumbi cha fani ya mbio za mita 10,000 wakati wa mashindano hayo kitaitwa “Naftali Temu 10,000m Classic”.

Kipchoge alijizolea nishani ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwenye Olimpiki za 1968 nchini Mexico kabla ya kutwaa medali nyingine ya dhahabu katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Olimpiki za 1972 jijini Munich, Ujerumani.

Kwa upande wake, Temu alitwalia Kenya nishani ya kwanza na ya mwisho katika mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki mnamo 1968 nchini Mexico. Kipchoge, Temu na Amos Biwott (mita 3,000 kuruka viunzi na maji), ndio Wakenya wa kwanza kunyakua medali za dhahabu kwenye Michezo ya Olimpiki mnamo 1968 nchini Mexico.

“Kipchoge ndiye baba wa Riadha za Kenya na dunia nzima inamfahamu zaidi kuliko Mkenya yeyote mwingine katika ulingo wa riadha,” akatanguliza Korir kwa kusisitiza kwamba kuita mbio za mita 10,000 ‘Naftali Temu’ kutachochea zaidi Wakenya kutamba katika fani hiyo wakati wa Olimpiki zijazo jijini Tokyo, Japan.

Mwingereza Mo Farah na Waethiopia ndio wamekuwa wakitawala mbio za mita 10,000 duniani kwa kipindi kirefu kilichopita.

RATIBA YA CONTINENTAL TOUR:

  • Paavo Nurmi Games (Turku, Finland, Agosti 11);
    • Istvan Gyulai Memorial (Szekesfehervar, Hungary, Agosti 19);
    • Seiko Golden Grand Prix (Tokyo, Japan, Agosti 23);
    • Kamila Skolimowska Memorial (Silesia, Poland, Septemba 6);
    • Ostrava Golden Spike (Ostrava, Czech, Septemba 8);
    • Memorial Borisa Hanzekivica (Zagreb, Croatia, Septemba 15);
    • Kip Keino Classic (Nairobi, Kenya, Septemba 26)
    • Nanjing Continental Tour (Nanjing, China, tarehe bado haijathibitishwa).