Michezo

Wanakandarasi wazembe wa viwanja waonywa

July 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KATIBU Msimamizi katika Wizara ya Michezo, Hassan Noor Hassan amesema kwamba muda wa makataa wa kukamilisha shughuli za ukarabati wa viwanja vya Kipchoge na Kamariny hautaongezwa.

Akizungumza jana katika uwanja wa Kipchoge alikokuwa akikagua maendeleo ya shughuli zinazolenga kuupa uwanja huo sura mpya, Hassan aliwaonya wakandarasi na akataka viwanja vyote vinavyokarabatiwa kwa sasa nchini vinastahili kukabidhiwa kwa Serikali Kuu na zile za Kaunti kufikia mwisho wa Septemba 2020.

Aidha, ilifichuka kwamba awamu ya kwanza ya ukarabati wa uwanja wa Kipchoge ilikwamizwa na mkandarasi wa China kwa sababu ya kesi dhidi yake ambayo kwa sasa inaendelea mahakamani.

Waziri wa Michezo, Amina Mohammed alikuwa ameweka makataa ya Septemba 20, 2020 kuwa siku ya mwisho kwa shughuli zote za ukarabati katika uwanja wa Kipchoge mjini Eldoret kukamilishwa rasmi.

Alisisitiza kwamba Serikali ilikuwa imetoa fedha zote zilizohitajika kwa shughuli hizo kukamilishwa chini ya kipindi hicho cha muda na hapakuwepo na sababu zozote kwa mkandarasi kutoafikia malengo hayo.

Mkandarasi anayekarabati wa uwanja wa Kamariny katika eneo la Iten, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet ametaka kupewa muda wa miezi minne zaidi ili kukamilisha shughuli za kuuboresha uga huo maarufu miongoni mwa wanariadha wa humu nchini.

Hassan amesisitiza kwamba serikali imejitolea kuwawekea wanamichezo wa humu nchini miundo-msingi bora katika juhudi za kuikuza sekta ya spoti.

“Kwa sasa tuna hazina ya fedha ya kutegemewa kutoka kwa serikali. Tunatarajia kukamilisha ukarabati wa sehemu iliyosalia ya uga wa Kamariny chini ya kipindi kifupi zaidi kijacho,” akasema Hassan.

“Tunafahamu kwamba wanariadha wa Elgeyo-Marakwet ni miongoni mwa wale ambao wamekuwa wakiipeperusha vyema zaidi bendera ya Kenya katika majukwaa ya kimataifa,” akatanguliza.

“Wamefaulu kufanya hivyo licha ya kutokea katika sehemu zisizo na miundo-msingi zozote za kufanikisha maandalizi yao kwa njia maridhawa, bila makocha wala akademia za kuwapokeza malezi yaafayo katika ulingo wa riadha,” akaongeza.