Cazorla kuhamia timu ya Xavi
Na CHRIS ADUNGO
KIUNGO wa zamani wa Arsenal, Santi Cazorla, yuko pua na mdomo kuingia katika rasmi ya kikosi cha Al Sadd nchini Qatar.
Cazorla, 35, aliwajibishwa katika mchuano wake wa mwisho kambini mwa Villarreal katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Julai 19, 2020 na mkataba wake kwa sasa umetamatika rasmi.
Kwa kujiunga na Al Sadd, Cazorla atakuwa sasa akinolewa na kiungo wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania, Xavi Hernandez, 40. Licha ya kuwaniwa pakubwa na Barcelona ambao wanalenga kumfuta Quique Setien na kuajiri kocha mpya msimu huu, Xavi alirefusha kipindi cha kuhudumu kwake kambini mwa Al Sadd hadi mwishoni mwa 2021.
“Tumeafikiana na Cazorla ambaye kwa sasa anakaribia kuwa mchezaji rasmi wa Al Sadd. Anatazamiwa kutua jijini Doha, Qatar wakati wowote kuanzia sasa kwa lengo la kurasimisha uhamisho wake kisha kutambulishwa kwa mashabiki na wachezaji wenzake,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Al Sadd.
Cazorla alichezea Arsenal jumla ya michuano 180 katika kipindi cha misimu sita kati ya 2012 na 2018. Amekuwa mwanasoka wa Villarreal kwa mara ya pili katika kipindi cha misimu miwili iliyopita.
Kiungo na nahodha wa Manchester City, David Silva, 34, pia anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea nchini Qatar kuvalia jezi za Al-Duhail.
Mnamo Juni 2020, Cazorla alitaka usimamizi wa Arsenal kumkubalia kurejea uwanjani Emirates atakapostaafu rasmi kwenye ulingo wa soka kusaidiana na kocha Mikel Arteta aliyekuwa mchezaji mwenza na ‘rafikiye mkubwa’ kambini mwa kikosi hicho ‘kuijenga’ upya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Hadi kuondoka kwake uwanjani Emirates mnamo 2018, Cazorla hakuwa amechezea Arsenal mchuano wowote tangu Oktoba 2016 kutokana na jeraha baya la misuli ya kifundo cha mguu.
Kubanduka kwake kimya kimya hakukustahiki mchezaji wa haiba yake aliyefunga jumla ya mabao 29 na kuchangia mengine 45 katika michuano 180 ndani ya jezi za Arsenal.
Akiwa Arsenal, Cazorla alisaidia kikosi hicho kutwaa mataji mawili ya Kombe la FA akicheza pamoja na Arteta ambaye amesema atakuwa radhi zaidi kuungana naye kwa mara nyingine katika ngazi ya ukocha.
Kuimarika kwa fomu ya Cazorla kila uchao ni miongoni mwa sababu zilizomshuhudia akipangwa katika timu ya taifa ya Uhispania kwa baadhi ya michuano ya kufuzu kwa fainali za Euro 2020 alizotamani sana kuzinogesha kabla ya kuangika daluga. Fainali hizo kwa sasa zimeahirishwa hadi 2021 kutokana na janga la corona.