Michezo

Wachezaji wawili tegemeo wagura City Stars

July 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KIPA Levis Opiyo na difenda Kevin ‘Chumsy’ Okumu wameagana rasmi na kikosi cha Nairobi City Stars kilichopandishwa ngazi hivi majuzi kushiriki Ligi Kuu ya Kenya msimu ujao wa 2020-21.

Afisa Mkuu Mtendaji wa City Stars, Patrick Korir amethibitisha kuondoka kwa wanasoka hao wawili baada ya kanadarasi zao kutamatika.

“Mikataba yao ilitamatika rasmi. Yalikuwa matarajio yetu kuwadumisha zaidi kikosini hasa ikizingatiwa ukubwa wa mchango wao katika kuturejesha kwenye Ligi Kuu. Hata hivyo, wamepania kutafuta hifadhi kwingineko kwa nia ya kukabiliana na changamoto mpya,” akatanguliza Korir.

“Kubanduka kwao baada ya kuwaniwa na klabu nyinginezo ishara kuimarika kwa makali yao wakiwa nasi. Inaridhisha sana kuona wachezaji wa City Stars wakijikuza kitaaluma kiasi hicho,” akasema.

Opiyo na Okumu wanahusishwa pakubwa na uwezekano wa kuingia katika sajili rasmi ya Gor Mahia.

Korir amefichua mipango ya City Stars kujishughulisha vilivyo kwenye soko la uhamisho na kujinasia huduma za wachezaji sita kwa minajili ya msimu ujao ili kujaza mapengo yaliyoachwa na baadhi ya wanasoka ambao wameagana nao.

City Stars tayari wanahemea maarifa ya kiungo Maurice Ojwang na beki Kelly Wesonga kutoka Western Stima ambao wapo katika hatari ya kuagana na idadi kubwa ya wachezaji baada ya kampuni ya umeme ya Kenya Power kukatiza udhamini wao.

Kati ya masogora wanaotarajiwa kukatiza uhusiano wao na Stima ni Wesonga, Fidel Origa, Ojwang na mfumaji chipukizi wa Harambee Stars, Benson Omalla.

Ingawa hivyo, mwenyekiti Laban Jobita amesisitiza kwamba uthabiti wao hautayumbishwa na tukio hilo kwa kuwa wanalenga kujisuka vilivyo baada ya muhula wa usajili wa wachezaji kufunguliwa rasmi.

“Tuna mpango wa kusajili chipukizi wengi watakaoongoza kampeni zetu zijazo. Stima haitamkwamilia mchezaji yeyote anayeazimia kutafuta hifadhi mpya kwingineko,” akatanguliza kinara huyo kwa kusisitiza haja ya klabu zinazovizia wanasoka wa Stima kuzingatia taratibu zilizopo za kusajili wachezaji.

“Wote wanaotaka kuagana nasi wako huru kufanya hivyo ila kwa kuzingatia taratibu zote zilizopo. Sera zetu hazituruhusu kumkwamilia mchezaji ambaye anahisi atapiga hatua kubwa kitaaluma akivalia jezi za kikosi kingine isipokuwa Stima,” akasema Jobita.

Wakati uo huo, kikosi cha Kisumu All Stars kimethibitisha kwamba kimekatiza uhusiano na kipa chaguo la kwanza Gad Mathews. Afisa Mkuu Mtendaji wa klabu hiyo, Nicholas Ochieng amesema All Stars wanalenga pia kuvunja ndoa kati yao na wanasoka sita zaidi.

Gad, 24, alisajiliwa na All Stars mnamo Januari 2020 kwa kandarasi ya miezi sita na akapata uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza. Kipa huyo wa zamani wa Wazito FC, tayari anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kusajiliwa na Tusker FC au kurejea kambini mwa Kariobangi Sharks.

All Stars wanatarajiwa kupepetana na Vihiga United waliomaliza kampeni za NSL katika nafasi ya tatu kubaini kikosi cha tatu kitakachoshuka daraja kwenye KPL na kitakachopanda ngazi kutoka NSL kwa minajili ya kinyang’anyiro cha msimu ujao wa 2020-21.