Corona: Wanavikapu wakwama
Na CHRIS ADUNGO
KUKOSEKANA kwa uhakika kuhusu kipindi cha kurejelewa kwa michezo ya humu nchini kumeathiri vibaya mipango ya kocha William Balozi wa kikosi cha vikapu cha Ulinzi Warriors.
Kwa mujibu wa Balozi, suitafahamu hiyo imewawia vigumu kurejelea mazoezi ya pamoja katika vikundi vidogo vidogo vya wachezaji kwa minajili ya kujindaa kwa kampeni za msimu mpya.
Aidha, mipango yao ya kujisuka upya upya kwa muhula ujao imetatizwa pakubwa kiasi kwamba kwa sasa hawezi kuanza mchakato wa kusajili wanavikapu anaowalenga wala kuwaachilia baadhi ya wachezaji ambao huduma zao hazihitajiwi na Ulinzi Warriors.
Anasema kikosi kinasubiri kwa hamu mwelekeo utakaotolewa na Waziri wa Michezo Amina Mohamed ambaye pia anasubiri kushauriwa na kamati ya watu 18 kutoa mwongozo kuhusu jinsi michezo ya humu nchini itakavyorejelewa.
Amina aliunda kamati hiyo yapata majuma mawili yaliyopita na ilistahili kuwasilisha rasmi mapendekezo yake kufikia Julai 10. Hata hivyo, makataa hayo hayakufikiwa na kamati ambayo ilihitaji muda zaidi kufikia idadi kubwa ya wadau kutoka sekta mbalimbali.
Ripoti ya kamati itatoa mwelekeo kuhusu jinsi shughuli za michezo zilizoahirishwa mnamo Machi 2020 kwa sababu ya corona zitakavyorejelewa na kanuni ambazo wanamichezo na mashabiki wanastahili kuzingatia.
“Ripoti ililenga kushughulikia jinsi michezo itakavyokuwa ikiendeshwa kwa mafanikio chini ya masharti yaliyotolewa na Wizara ya Afya kuhusu namna ya kudhibiti maambukizi zaidi ya ugonjwa wa Covid-19,” akatanguliza.
“Itatueleza ni watu wangapi wanastahili kushiriki na kuhudhuria aina mbalimbali ya michezo, kiwango cha kuhusishwa kwa idara nyinginezo za serikali na mchango ambao unafaa kutolewa na wizara hizo husika ili kufanikisha uendeshaji wa michezo ambayo imesitishwa kwa miezi minne iliyopita,” akaongeza Amina.
Kauli ya kocha Balozi imeungwa na kocha wa kikosi cha wanavikapu wa kike wa KPA Mike Opel, mkufunzi wa timu ya wanavikapu wa kiume ya Equity Bank, Carrey Odhiambo na kocha wa timu ya Chuo Kikuu cha KCA Victor Okello ambao pia wanasubiri mwelekeo wa serikali kabla ya kufichua mipangilio yao ya mazoezi na usajili.
“Kwa sasa tumesitisha kila kitu yakiwemo masuala ya mazoezi, ununuzi na uuzaji wa wachezaji,” akasema Balozi aliyewaongoza Ulinzi Warriors kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Vikapu msimu uliopita.
Msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vikapu ulitazamiwa kuanza Machi 2020 ila ukasitishwa kwa muda kutokana na janga la Covid-19 lililovuruga kalenda ya michezo mbalimbali ya humu nchini na dunia nzima.
“Tunasubiri kujua mapendekezo ya kamati iliyoundwa na wizara ya michezo kabla ya kufahamu hatua za kupiga.
“Maazimio yetu ni kukifanyia kikosi mabadiliko makubwa ambayo kwa sasa hatuwezi kutekeleza kwa sababu ya athari za corona. Isitoshe, hatujui kitakachoaamuliwa na serikali baada ya mapendekezo ya kamati ya kuishauri kutolewa,” akasema Opel.
“Hatuna uhakika iwapo tutarejelea michezo mwaka huu. Hata hivyo, wanavikapu wangu wanajifanyia mazoezi na ninafuatilia sana maendeleo ya kila mmoja wao kupitia mtandao wa WhatsApp. Tunatumia jukwaa hilo kubadilishana video na kutoa ushauri ufaao kwa wanakikosi,” akasema Odhiambo.