HabariSiasa

Joho awindwa na EACC

July 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

MOHAMED AHMED na FARHIYA HUSSEIN

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inachunguza madai ya ufujaji wa pesa katika Serikali ya Kaunti ya Mombasa inayoongozwa na Gavana Hassan Joho.

Mkuu wa EACC jijini Mombasa, Bw Mutembei Nyaga jana alithibitisha kupokea ripoti kutoka kwa madiwani wa kaunti hiyo kuhusu utawala wa Bw Joho, ambaye ni mmoja wa wandani wakuu wa Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Bw Nyaga alisema EACC itaamua hatua Za kuchukua baada ya kuchunguza madai yaliyowasilishwa, ambayo yanahusu utumiaji mbaya wa takribani Sh30 bilioni zilizokuwa kwa bajeti ya kaunti tangu 2017.

Haya yamefichuka siku chache baada ya kubainika kuwa Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed, pia anaandamwa na makachero wa EACC kuhusu kashfa ya ufisadi katika Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS) iliyotokea mnamo 2015.

“Tulipokea barua hiyo juzi na bado tunaangalia madai hayo kutoka kwa madiwani,” akasema Bw Nyaga.

Katika barua yao kwa EACC, madiwani wanadai kumekuwa na ubaridhifu wa fedha katika utekelezaji wa bajeti za kaunti kuanzia 2017.

Wakiongozwa na Diwani wa Wadi ya Mjambere, Bw Fahad Kassim pamoja na mwenzake wa Frere-Town Charles Kitula, waliitaka EACC kuhakikisha usimamizi wa kaunti unapeana ripoti zake za fedha bungeni ipasavyo.

‘Tulimpa gavana muda atueleze jinsi pesa zilitumiwa. Tuliomba pia Idara ya Fedha kupitia kwa mwenyekiti wake itupatie angalau sababu ya kuridhisha kuhusu jinsi pesa zilitumiwa lakini hatujawahi kujibiwa hadi sasa. Tunasema tumechoka, wacha EACC ishughulikie hilo suala,’ akasema Bw Kitula.

Bw Kassim alidai kaunti hiyo ilikuwa inapanga kutumia Sh64 milioni kuweka maua katika kaunti na Sh3.4 milioni nyingine kuchimba visima akisema pesa hizo ni nyingi kwa miradi hiyo.

Kando na kupeleka kesi kwa EACC, walitishia kuwasilisha hoja ya kumng’oa Bw Joho mamlakani wakisema, pesa hutengewa maendeleo kwenye bajeti lakini hakuna miradi inaonekana mashinani.

“Kwa miaka mitatu hakujakuwa na uwasilishaji wa ripoti kuhusu matumizi ya fedha bungeni kama inavyotakikana kisheria,” akasema Bw Kassim kwenye mahojiano.

Aidha, viongozi hao wameitaka afisi ya fedha za kaunti kuhakikisha kuwa ripoti za fedha zinatumwa bungeni na kupelekwa katika afisi za serikali kuu kama inavyotakikana.

Viongozi hao wamedai hilo halitekelezwi ipasavyo kwa sababu ya njama za kuficha matumizi ya fedha za umma.

Uwasilishaji ripoti hizo ni hitaji la kisheria ambalo linapaswa kutekelezwa na kila kaunti nchini; jambo ambalo wawakilishi wa Mombasa wanadai halijakuwa likitekelezwa.

“Mambo yanafanywa tofauti hapa na ndio sababu hatuna imani na kamati ya fedha ambayo ndio imekuwa ikichangia kuwepo kwa shida hizi zote,” akasema Bw Kassim.

Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati ya fedha katika bunge la kaunti, Bw Mohammed Hatimy amepinga madai ya madiwani hao akisema hayana msingi. A

lisema ripoti hizo ambazo madiwani hao wanataka zimekuwa zikipelekwa katika afisi za wakuu wa fedha jijini Nairobi kama inavyotakikana.

“Serikali kuu inapata ripoti za kaunti kupitia kwetu, na bunge limekuwa likiwasilisha ripoti hizo ndio maana hakujakuwa na shida yoyote na afisi za serikali kuu zinazoangalia masuala ya fedha,” akasema Bw Hatimy.

Alieleza kuwa, pesa za kaunti zimekuwa zikitumiwa vyema kwa miradi ya maendeleo na kulipa mishahara ya wafanyakazi.

‘Kuna miradi katika kaunti, ilhali wanadai hakuna chochote kimefanywa. Pesa hutumiwa pia kulipa wafanyakazi mishahara yao miongoni mwa mahitaji mengine,’ akasema.