Tahadhari katika ofisi za serikali corona ikienea
Na WAANDISHI WETU
SHUGHULI nyingi za serikali zinakabiliwa na hatari ya kukwama baada ya virusi vya corona kupenya katika ofisi za umma na kuathiri huduma.
Tayari mkuu wa Utumishi wa Umma, Bw Joseph Kinyua, ameagiza idara na mashirika ya serikali kupunguza shughuli na wageni wanaotembelea ofisi za umma+.
Bw Kinyua alisema ni wafanyakazi wanaotekeleza huduma muhimu wanaofaa kuwa katika ofisi huku walio na matatizo ya kiafya na umri mkubwa wakitakiwa kufanya kazi wakiwa nyumbani.
Hatua hiyo imesababishwa na kuongezeka kwa idadi ya wafanyakazi wa umma wanaoambukizwa virusi hivyo wakiwemo wahudumu wa afya.
Bw Kinyua alitoa agizo hilo huku magavana wakisema kwamba wanahofia maelfu ya watu watauawa na virusi vya corona iwapo wizara ya fedha itachelewesha mgao wa Sh30 bilioni kwa kaunti zote 47.
Kufikia Jumatano, jumla ya watu 260 walikuwa wamefariki kutokana na ugonjwa huo baada ya vifo vipya 10 kuripotiwa.
Wizara ya Afya ilitangaza kuwa visa vipya 637 vilithibitishwa Jumanne na kufikisha 14,805 visa vya maambukizi ya corona nchini.
Mwenyekiti wa baraza la magavana, Bw Wycliffe Oparanya, ambaye pia ni Gavana wa Kakamega, alimtaka Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani atoe fedha hizo ambazo zinahitajika sana kusaidia katika vita dhidi ya virusi hivyo na masuala mengine ya maendeleo.
“Vita dhidi ya janga hili vitaathirika pakubwa iwapo kaunti hazina rasilimali za kutosha. Hii huenda ikachangia vifo kwa sababu serikali za kaunti hazitakuwa na uwezo wa kufanikisha vita hivyo kivyao,’ akasema Bw Oparanya.
Pia kwenye barua aliyoandikia Bw Yattani, Bw Oparanya alisema huduma nyingine kwenye kaunti zitaathirika iwapo mgao huo utachelewa kufikia kaunti zote 47.
“Tunatambua kwamba kuna upungufu wa fedha kwa sasa kutokana na janga la virusi vya corona. Hali hii ndiyo imechangia tatizo la serikali kuchelewa kutuma mgao wa fedha kwa kaunti mwaka wa kifedha 2020/21 na kuchelewesha pia Sh30 bilioni za mwezi Julai. Hata hivyo, tunaomba uingilie suala hili ili fedha hizi zifikie kaunti,” akasema.
Baraza la magavana lilimuomba Rais Uhuru Kenyatta kuahirisha kikao nao Ijumaa kujadili jinsi kaunti zimejiandaa kukabiliana na maambukizi yanayozidi kuongezeka na kutia hofu.
Ikulu ya Nairobi ilisema kwamba Rais Kenyatta alikubali ombi hilo na kuahirisha mkutano huo hadi Jumatatu Julai 27.
Kwenye taarifa, Bw Oparanya alisema kufunguliwa kwa kaunti za Nairobi, Mombasa na Mandera, kumeongeza mzigo kwa kaunti nyingine.
Hata hivyo alisema serikali za kaunti zinajitahidi ikiwa ni pamoja na kukumbatia mfumo wa kuuguza wagonjwa nyumbani. Kwa sasa, kaunti zinakabiliwa na wakati mgumu kuendesha masuala yao ikizingatiwa hazina Kuu ya kifedha bado haijatoa Sh30 bilioni za mwezi Julai.
Baadhi ya kaunti zimepitisha bajeti zao za kila mwaka kwa matumaini kwamba zitapokezwa mgao huo.
Mwenyekiti wa Muungano wa Mabunge ya Kaunti (CAF), Bw Ndegwa Wahome, ambaye pia ni Spika wa kaunti ya Nyandarua, alisema kucheleweshwa kwa fedha hizo kutaathiri sana kaunti zote 47.
“Ingawa hatuwezi kusema serikali kuu imefeli kwa sababu hata mapato yanayotokana na ushuru hayatoshi kuendesha shughuli zote. Serikali inahitaji tu kupunguza fedha zilizotengewa huduma ambazo hazina umuhimu mkubwa,” akasema Bw Wahome.
Juhudi za Taifa Leo kumfikia Bw Yattani ziligonga mwamba kwa kuwa hakupokea simu au kujibu jumbe zetu. Wakati huo huo, jana, idara ya mahakama ilifunga mahakama ya Makadara jijini Nairobi, baada ya wafanyakazi wawili kuambukizwa virusi vya corona.
Kwenye taarifa, Msajili Mkuu wa Mahakama, Bi Anne Amadi, alisema mahakama hiyo itafungwa kwa siku 14 ili iweze kupuliziwa dawa.
Mahakimu na wafanyakazi wote waliagizwa kujitenga. “Tumeagiza kuwa mahakama hiyo ifungwe kwa siku 14 na mahakimu na wafanyakazi wote wajitenge nyumbani mara moja,” Bi Amadi alisema kwenye taarifa.
Mahakama ya Milimani itafungwa kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu ili ipuliziwe dawa. Alisema wafanyakazi waliothibitishwa kuwa na corona hawana dalili za ugonjwa huo.
Taarifa ya FRANCIS MUREITHI, MARY WANGARI Na BENSON MATHEKA