• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:21 PM
‘Serikali imefumbia macho magonjwa mengine hatari’

‘Serikali imefumbia macho magonjwa mengine hatari’

Na SAMMY WAWERU

Ugonjwa wa Covid-19 ambao sasa ni janga la ulimwengu mzima umeathiri sekta mbalimbali kwa kiasi kikuu.

Kuanzia sekta ya biashara, utalii, uchukuzi, kilimo, kati ya nyinginezo zinapitia nyakati ngumu.

Kimsingi, uchumi unaendelea kukandamizwa na kupunjwa na ugonjwa huu unaosababishwa na virusi hatari vya corona.

Sekta ya afya na ambayo kwa sasa ndiyo tegemeo kuu, imeonekana kulemewa na makali ya corona, zaidi ya wahudumu 500 wa afya wakithibitishwa kuambukizwa virusi.

Huku serikali ikielekeza nguvu zake kupambana na Covid-19, imeonekana kupuuza maradhi mengine hatari kama vile Malaria, Kifua kikuu, Kipindupindu, Homa ya Matumbo, miongoni mwa mengineyo.

Katika vingi vya vituo vya afya unapovizuru kutafuta matibabu, vipimo vya kwanza wanavyofanya ni virusi vya corona, na kuonekana kupuuza magonjwa mengine.

Ni matukio yanayodhihirika wazi kufuatia kifo cha mwigizaji wa vipindi vya runinga maerehemu Charles Bukeko, ambapo familia yake inalaumi Hospitali ya Karen, Nairobi kwa kukataa kufanya vipimo vya magonjwa mengine.

Kulingana na mkewe Beatrice Andega, Bukeko aliyefahamika kwa jina la uigizaji kama Papa Shirandula aliomba afanyiwe uchunguzi wa magonjwa matatu ambayo ni Malaria, Kifua Kikuu (Niumonia) na Covid-19.

“Tulipoenda katika hospitali hiyo aliomba afanyiwe uchunguzi wa magonjwa matatu ambayo ni Malaria, Niumonia na Covid-19 lakini ilipima corona pekee na kukataa kupima mengine,” Beatrice akaambia waombolezaji wakati wa mazishi ya Bukeko mnamo Jumatatu Julai 20, 2020, eneo la Funyula, Kaunti ya Busia.

Familia hiyo ikiongozwa na babake Bukeko, Cosmas Wafula na mkewe Beatrice Andega inataka Hospitali ya Karen kutoa taarifa ya kina kuhusu kifo cha mwigizaji huyo anayeendelea kuombolezwa na Wakenya kufuatia mchango wake mkuu katika tasnia ya uigizaji nchini.

Hata hivyo, hospitali hiyo kupitia taarifa kwa vyombo vya habari ilipuuzilia mbali madai ya familia hiyo, ikisema Hospitali ya Karen inasifika kwa utoaji huduma za hali ya juu kwa wagonjwa.

Kwenye taarifa hiyo, ilisema wahudumu wake wanaendelea kutoa huduma bora kwa Wakenya hata wakati huu wa janga la Covid-19, huku wakizingatia kanuni za Wizara ya Afya na Shirika la Afya Ulimwenguni.

Familia ya Papa Shirandula imesema itaelekea mahakamani kutafuta haki.

Utepetevu wa hospitali hiyo umezua mdahalo mkali mitandaoni, Wakenya wachangiaji wakiikashifu kwa kile wanasema ni kutojali maisha na uhai wa wanyonge.

“Kwa sasa nimeamini malalamishi ya mke wa Papa, haiwezi (Hospitali ya Karen) kuzuia uhuru wa kueleza maoni ya haki,” Mwanablogu Robert Alai anaeleza kwenye ukurasa wake wa Facebook, chapisho ambalo limeibua mjadala Wakenya wakitoa hisia za ghadhabu kwa idara ya afya nchini.

“Sekta yetu ya afya ilioza kitambo na ndio maana hata maafisa wakuu serikalini hawana imani nayo, hutafuta matibabu nje ya nchi,” alalamika Trump Eddy Mc’owitch.

“Iwache ukiritimba, iombe familia ya Papa msamaha. Kuwa daktari kunahitaji mapenzi ya dhati ila si kuongozwa na tamaa ya pesa,” Sophie Ouma Oyuba anaikashifu Hospitali ya Karen.

Kulingana na maelezo ya mke wa Papa Shirandula, Beatrice Andega, Bw Bukeko alikawishwa katika eneo la kupokea wagonjwa akisubiri matokeo ya vipimo hadi kufariki kwake.

Masaibu na kisa cha kuhuzunisha cha marehemu Bukeko ni taswira ya yanayoendelea katika vituo mbalimbali vya afya nchini, hasa wakati huu wa corona.

Ni ishara kuwa serikali imeelekeza macho yake na raslimali zake kwa janga hili, na kusahau kuna majanga ya magonjwa mengine hatari na ambayo yanaua kwa kasi.

Si ajabu kugundua baadhi ya maafa yanayosababishwa na ugonjwa wa Malaria, Niumonia, Kisukari, Moyo, na mengineyo yakisemekana ni corona.

Mtu anapougua homa ya kawaida imlemee, atafute matibabu hospitalini, hofu inayomgubika ni kuhusishwa na Covid-19.

Isitoshe, ni suala ambalo limesababisha wananchi kuchelea kuenda hospitalini wakiogopa kupimwa corona na pia kujitia katika hatari ya kuambukizwa virusi hivyo hatari.

Ni muhimu serikali ifahamu, mbali na janga la Covid-19, magonjwa mengine hatari pia ni janga na ambayo yanaendelea kuangamiza watu.

You can share this post!

Visa 5,000 vya dhuluma za kijinsia vyaripotiwa

Aibu duniani wanariadha Wakenya wakizidi kutumia pufya

adminleo