Mpango wa kubatilisha KPL iwe FKFPL
Na CHRIS ADUNGO
WENYEVITI wa klabu kuu za soka ya Kenya wamechagua Dan Shikanda, Robert Maoga, Daniel Aduda, Erick Oloo na Ken Ochieng kuwa vinara wa kamati itakayosimamia mchakato utakaoshuhudia Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ikibadilishwa jina na kuitwa Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKFPL).
Watano hao kwa sasa ni wenyeviti wa vikosi vya AFC Leopards, Kariobangi Sharks, Tusker, Ulinzi Stars na Zoo Kericho FC mtawalia.
Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kutoa mapendekezo kuhusu jinsi FKFPL itakavyoendeshwa baada ya kutamatika kwa kandarasi ya kampuni ya KPL mnamo Septemba 2020.
Kamati itatalii pia uwezekano wa klabu zote zinazoshiriki soka ya Ligi Kuu ya Kenya kupiga kura ya kumchagua mwenyekiti huru atakayesimamia shughuli za uendeshaji wa ligi kupitia FKFPL.
Wanakamati hao watakuwa pia na jukumu la kushauri Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuhusu utaratibu za kuboresha zaidi usimamizi wa kabumbu ya humu nchini tofauti kabisa na jinsi ilivyokuwa ikiendeshwa na KPL.
Uteuzi wa wanakamati hao watano uliidhinishwa na klabu 10 kati ya 17 za Ligi Kuu ya Kenya kupitia mkutano wa mtandaoni uliohudhuriwa na wenyeviti 16 wa vikosi vya Ligi ya KPL kwa pamoja na Rais wa FKF, Nick Mwendwa.
Mwenyekiti wa Mathare United Bob Munro, Cleophas Shimanyula (Kakamega Homeboyz), Evance Kadenge (Nzoia Sugar), Edward Oduor (Bandari FC) na kinara wa Wazito FC aliyekuwa akimwakilisha mwenyekiti Ricardo Badoer walipiga kura dhidi ya wenzao watano waliochaguliwa kusimamia kamati mpya ya FKFPL.
Wakili Ambrose Rachier ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa KPL hakushiriki kikamilifu mkutano huo. Mbali na kutochangia hoja yoyote wakati wa mkutano, hakushiriki shughuli ya upigaji kura, kuuliza swali wala kujibu. Elly Kalekwa ambaye ni mwenyekiti wa Sofapaka, hakuhudhuria kabisa mkutano huo ulioagizwa na Mwendwa.
Zaidi ya kuchagua kamati ya mpya ya mpito, wenyeviti wa vikosi vya Ligi Kuu ya soka ya humu nchini walielezewa kuhusu mpango mpya wa udhamini kati ya FKF na kampuni ya kamari ya BetKing kutoka Nigeria.
BetKing inatazamiwa kufadhili soka ya Ligi Kuu ya Kenya kwa kima cha Sh1.2 bilioni kwa miaka mitano ijayo. FKF imethibitisha kwamba mpango huo utashuhudia kila kikosi cha Ligi Kuu ya FKFPL kikipokezwa Sh8 milioni kwa msimu.
BetKing pia itafadhili soka ya daraja la tatu ya Divisheni ya Kwanza kwa Sh100 milioni. Mpango huo utaendeshwa kwa miaka mitano ijayo huku kila kikosi kitakachoshiriki kivumbi hicho kikipokezwa Sh500,000 kwa mwaka.
“Hii ni mara ya kwanza katika historia ya soka ya Kenya kwa soka ya daraja la tatu ya Divisheni ya Kwanza kupata mdhamini. Ni hatua nyingine kubwa katika maendeleo ya soka yetu pamoja na makuzi ya thamani yake,” akasema Mwendwa.
Kufaulu kwa mpango huo wa udhamini kwa sasa unamaanisha kwamba washiriki wote wa madaraja matatu ya soka ya Kenya wanafadhiliwa na kampuni za mchezo wa kamari. Kampuni ya Betika ndiyo inayodhamini Ligi ya Kitaifa ya Daraja la Pili (NSL) huku Odibets ikifadhili ligi za soka ya mashinani.
Klabu zote za Ligi Kuu ya soka ya Kenya zilizounga mkono dili kati FKF na BetKing na kutia saini mwafaka huo, zinatarajiwa kupokezwa leo Sh500,000 za kwanza. Haya ni kwa mujibu wa wenyeviti waliohudhuria mkutano kati yao na Mwendwa.
Mwendwa alithibitisha mkutanoni kwamba BetKing tayari imetia Sh12 milioni kwenye akaunti za benki za FKF na ni suala la muda tu kabla ya fedha zinazohitajika kuanza kutolewa kwa klabu husika za Ligi Kuu.
BetKing inatarajiwa kuweka Sh75 milioni katika akaunti za FKF mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa kampeni za msimu mpya na kiasi hicho cha fedha kabla ya mwisho wa mwezi wa tatu wa kampeni za muhula ujao wa 2020-21. Klabu zitapokezwa mgao wa mwisho wa jumla ya Sh8 milioni kwa msimu kufikia mwezi wa sita wa kampeni.