Michezo

Emery apewa kazi ya kunoa Villarreal

July 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa zamani wa Arsenal na Paris Saint-Germain (PSG) amepokezwa rasmi mikoba ya kikosi cha Villarreal kinachoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania.

Emery, 48, ameajiriwa kwa mkataba wa miaka mitatu. Anajaza nafasi ya mkufunzi Javi Calleja aliyebanduka kambini mwa Villarreal mwishoni mwa msimu huu wa 2019-20 licha ya kuwaongoza waajiri wake hao kutinga nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Ufanisi huo wa Villarreal unawakatia tiketi ya kushiriki kivumbi cha Europa League msimu ujao wa 2020-21.

Emery ambaye ni mzawa wa Uhispania, hajakuwa na kikosi cha kunoa tangu Novemba 2019 alipotimuliwa na Arsenal baada ya kuwahudumia uwanjani Emirates kwa kipindi cha miezi 18 pekee.

Mbali na PSG (Ufaransa) na Arsenal (Uingereza), Emery anejivunia pia kuwahi kutia makali vikosi vya Sevilla na Valencia katika kipute cha La Liga.

Emery aliaminiwa kuwa mrithi wa kocha Arsene Wenger kambini mwa Arsenal mnamo Mei 2018 baada ya kuwaongoza Sevilla kutia kapuni mataji matatu mfululizo ya Europa League na ubingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) akidhibiti mikoba ya PSG.

Kutimuliwa kwake na Arsenal kulichangiwa na msururu wa matokeo duni zaidi ya kikosi hicho kwa kipindi cha miaka 27.