Michezo

Pioli apewa miaka 2 kuboresha AC Milan

July 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Stefano Pioli wa AC Milan amerefusha muda wa kuhudumu kwake kambini uwanjani San Siro kwa kipindi cha miaka miwili zaidi hadi mwishoni mwa Juni 2022.

Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 54 alipokezwa rasmi mikoba ya AC Milan mnamo Oktoba na mkataba wake wa awali unakamilika mwishoni mwa msimu huu.

Chini ya ukufunzi wake, Piolo ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Lazio na Inter Milan, kikosi cha AC Milan kinajivunia kwa sasa nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na kipo pua na mdomo kufuzu kwa kivumbi cha Europa League msimu ujao.

“Nimefurahishwa na ukubwa wa imani ambayo Milan wanayo kwangu. Namshukuru kila mtu, wakiwemo mashabiki wetu ambao tunazidi kuwakosa sana uwanjani. Usimamizi umeniunga mkono vilivyo na nina uhakika tutafaulu zaidi tukidumisha ushirikiano huu ambao umekuwa mhimili wa ufanisi wa hadi kufikia sasa,” akasema Pioli.

“Stefano amedhihirisha kwamba ana uwezo mkubwa wa kutushindia mechi muhimu, kututambisha ligini na kuturejeshea hadhi ya awali iliyokuwa kitambulisho cha Milan,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Milan, Ivan Gazidis.

AC Milan wangali na michuano mitatu zaidi ya kusakata kabla ya kampeni za msimu huu katika Serie A kutamatika rasmi. Wamepangiwa kuvaana na nambari tatu Atalanta uwanjani San Siro mnamo Ijumaa ya Julai 24, 2020.