Wito makocha wafuatilie wanasoka wao
Na CHRIS ADUNGO
LICHA ya kalenda ya michezo mbalimbali msimu huu kuvurugwa na ugonjwa wa Covid-19, kocha David Ouma amefichua kwamba amekuwa akifuatilia maendeleo ya wanasoka wake wa Harambee Starlets kupitia makocha wa klabu zao.
Chini ya Ouma, Starlets walikuwa wameratibiwa kuvaana na Tanzania mnamo Agosti 2020 katika raundi ya kwanza ya mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON). Hata hivyo, kipute hicho kilifutiliwa mbali na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) katika kikao cha Juni 30.
Ni katika mkutano huo ambapo CAF pia ilizindua mashindano ya Klabu Bingwa na Kombe la Mashirikisho barani Afrika miongoni mwa wanawake katika kiwango cha klabu na ngazi ya timu za taifa.
Utaratibu wa kubaini washiriki wa kiwango cha timu za taifa utatolewa na CAF wiki ijayo. Kenya itawakilishwa na Vihiga Queens katika makala ya kwanza ya mapambano ya Klabu Bingwa (CAF Champions League) mwakani katika ngazi ya klabu. Vipusa hao wa kocha Alex Alumira waliibuka mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KWPL) msimu huu wa 2019-20.
“Kampeni hizi za Klabu Bingwa Afrika zitatoa jukwaa mwafaka zaidi kwa vipusa wetu kuvaana na vikosi bora barani Afrika, na hivyo kuimarisha viwango vya maendeleo ya mchezo huu,” akasema Ouma katika kauli iliyoungwa na Alumira ambaye ni mshindi mara tatu wa taji la KWPL.
Ouma amefichua kwamba Kenya inapigiwa upatu wa kuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Afrika la soka ya ufukweni kwa wanawake (Beach Soccer Cup of Nations) mwaka ujao baada ya Uganda waliokuwa wametwikwa uandalizi kujiondoa.
CAF inawazia pia uwezekano wa Kenya au Morocco kupokezwa uenyeji wa fainali za Kombe la Afrika kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17 mnamo Julai 2021 baada ya Rwanda kujiondoa.
“Nahimiza wakufunzi wa klabu mbalimbali waendelee pia kufuatilia mazoezi ya wachezaji wao nyumbani kadri wanavyozidi kujiandaa kwa mapambano yajayo ya CAF,” akasema Ouma kwa kusisitiza kwamba amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na wachezaji wake, hasa wanasoka aliowategemea katika kivumbi kilichopita cha Turkish Cup.
Ouma aliwaongoza Starlets kusajili matokeo ya kuridhisha katika kampeni za kufuzu kwa Olimpiki za Tokyo, Japan kabla ya kubanduliwa na Ghana. Isitoshe, vipusa wake walitawazwa mabingwa wa Cecafa 2019.
Ufanisi huo ulichangia kipa Annette Kundu na beki Ruth Ingosi waliokuwa wakichezea Eldoret Falcons kusajiliwa na Lakatamia FC ya Cyprus huku Corazone Aquino akiyoyomea Ureno kuvalia jezi za Atletico Ouriense. Cynthia Shilwatso na Mwanahalima Adam pia wako mbioni kujiunga na EDF Logrono na Djugardens IF nchini Uhispania na Uswidi mtawalia.