HabariSiasa

Kenya yamwomboleza Benjamin Mkapa

July 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Ijumaa aliongoza Wakenya kuomboleza kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Benjamin Mkapa.

Kiongozi huyo, aliyeongoza Tanzania kati ya 1995 na 2005, alifariki Alhamisi usiku katika Hospitali ya Dar es Salama alikolazwa baada ya kuugua.

Katika risala zake, Rais Kenyatta alimtaja Mkapa kama kiongozi mashuhuri ambaye alijitolea “kwa ajili ya kufanikisha ndoto ya uwepo wa utangamano, amani na maendeleo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.”

“Tanzania, Kenya na eneo zima la Afrika Mashariki litamkosa kiongozi huyu shupavu aliyekuwa kielelezo kwa viongozi wengi Afrika na ulimwengu kwa ujumla,” akaeleza.

Rais mstaafu Mwai Kibaki alisema marehemu Mkapa ni kiongozi aliyejijengea himaya ya sifa kama mpatanishi mkuu aliyeheshimika katika eneo zima la Afrika Mashariki.

“Kando na kuwa mpatanishi, Mkapa atakakumbukwa kuleta sera ya uchumi huru nchini Tanzania, hali iliyoleta mwamko mpya nchini humo,” Mzee Kibaki akasema kwenye taarifa. Alimtaja mwendazake kama rafiki mkubwa wa mwanzilishi wa taifa la Tanzania Mwalimu Juliua Kambarage Nyerere.

Baada ya kuondoka uongozini Mkapa amewahi kushiriki mazungumzo ya amani katika mataifa kama vile Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zimbabwe, Burundi na Kenya.

Naye kiongozi wa ODM Raila Odinga alimtaja Mkapa kama rafiki mkubwa wa Wakenya na kiongozi mtetezi wa masilahi ya bara la Afrika.

“Mkapa alienzi utangamano wa kikanda na alitetea kufufuliwa kwa Jumuiy ya Afrika Mashariki (EAC) mnamo 1999. Kifo chake kimelipokonya Afrika,” akasema Bw Odinga.

Viongozi wengine walioamboleza marehemu Mkapa ni Naibu Rais William Ruto, Gavana wa Kisumu Peter Anyang’ Nyong’o na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.