CHOCHEO: Ni sawa kumwambia mpenzi wako siri zote?
NA BENSON MATHEKA
Selina hakuweza kuficha hasira zake alipogundua kuwa Jimmy hakumweleza ukweli kuhusu maisha yake ya mapenzi kabla ya kuoana.
Alimkaripia na kutisha kuvunja ndoa yao akimlaumu kwa kutokuwa mwaminifu. Alisema aligundua Jimmy alikuwa amemtema mpenzi wake wa awali baada ya kumpachika mimba.
Kilimchomuudhi hata zaidi ni kwamba alikuwa amemfichulia Jimmy alivyotengana na mpenzi wake wa awali kwa sababu ya kubania siri zake.
“Huyu si mwanamume mwaminifu. Ikiwa anaweza kumtema mwanamke baada ya kumpachika mimba na zaidi ya yote akose kunieleza ilhali tuliahidiana kuambiana ukweli kuhusu maisha yetu ya awali ya mapenzi, ni mambo mangapi atanificha tukiwa mume na mke?”alihoji Selina
. Ingawa Jimmy alimuomba msamaha akisema alimtema mwanadada huyo baada ya kugundua alikuwa akitoka na wanaume wengi na alishuku mimba haikuwa yake, Selina hakuweza kumwamini.
Naye Liza, mwenye umri wa miaka 27 asema hawezi kujisamehe kwa kutomweleza ukweli mpenzi wake.
“Mike alikasirika alipogundua nilimficha kwamba nilikuwa mhudumu wa baa. Hilo lilifanya uhusiano wetu kuingia doa,” asema Liza.
Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema kwamba kuna siri zinazoweza kuvuruga uhusiano wa kimapenzi hasa mtu akikosa kufungua roho kuhusu maisha yake ya awali ya mapenzi.
“Kuna mambo ambayo mtu anafaa kuweka wazi kabla ya kuanza uhusiano wa kimapenzi. Ikiwa ulikuwa na uhusiano wa awali, usimfiche mpenzi wako mpya hasa ikiwa mnapanga kuoana.
Mweleze ukweli kuhusu kilichofanya uhusiano huo kuvunjika na aliko mpenzi wako wa awali. Kuficha ukweli kuhusu maisha yako ya awali ya mapenzi ni kuweka msingi mbaya wa uhusiano mpya,” asema David Sino, mshauri wa kituo cha Abundant Love, jijini Nairobi.
Anasema ni makosa mtu kugundua kwamba mchumba wake alikuwa na watoto na mwanamke mwingine na hakumfahamisha.
“Pasua mbarika wewe mwenyewe. Usisubiri mtu wako apate uhondo kutoka kwa wambea mtaani,” asema Sino.Wataalamu wanasema ingawa sio lazima mtu afichue siri zote, kuna zile ambazo zikifichuka zinaweza kusambaratisha uhusiano.
“Kwa mfano, mwanamke hawezi kuficha mtoto aliyezaa na mwanamume mwingine. Inashangaza baadhi ya wanawake hukosa kueleza wanaume wanaowatongoza kwamba wa0na watoto,” aeleza Sino.
Wanasaikolojia wanasema kwamba watu wanafaa kupima wanayofichulia wachumba wao na wakati wa kufanya hivyo.
“Kuna siri zinazoweza kufedhehesha mtu au kutia doa uhusiano. Pia, kuna zile unazofaa kufichua katika vipindi fulani vya uhusiano. Inahitaji hekima kufanya hivyo,” aeleza Dorcas Sossy, mwanasaikolojia wa shirika la Maisha Mema, jijini Nairobi.
Jonathan Bennett, mtaalamu wa shirika la Double Trust anakubaliana na Sossy kwamba watu hawafai kuanika mara moja maisha yao ya mapenzi ya awali kwa wachumba wao.
“Kuna mambo ambayo unafaa kuweka chini ya maji ukihisi kwamba ni ya aibu na yanaweza kukuletea majuto. Kuna mambo ambayo una hakika mchumba wako hatayang’amua,” asema Jonathan.
Mtaalamu huyu anasema mtu anafaa kuwa na uhuru wa kuamua siri za kufichulia mchumba wake.
“Huwa ninashauri wachumba kujadili suala hili na kukubaliana kwa sababu huwa linazua migogoro,” aeleza.
Sinyo anashauri watu kutowaficha wachumba matatizo ya afya yanayowasumbua. “Ikiwa uko na shida ya kiafya kama kisukari au hata shinikizo la damu, mweleze mtu wako. Kwa kufanya hivi, utajua kama anakupenda kwa dhati, aeleza.
“Kuwa mkweli kuhusu masuala haya kwa sababu sio ya muda mfupi na ikiwa anakupenda kwa dhati atakupa moyo na kuwa katika hali nzuri ya kukufaa mkioana,” asema Sino.
Hata hivyo watalaamu wanasema kwa watu wengi huwa ni vigumu kuwaeleza wachumba wao maisha yao ya awali ya mapenzi hasa ikiwa walikuwa na wachumba wengi.