• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Atumia ubunifu wake kuunda mtambo wa kunawa mikono

Atumia ubunifu wake kuunda mtambo wa kunawa mikono

Na SAMMY WAWERU

Udumishaji wa kiwango cha juu cha usafi ni miongoni mwa mikakati iliyoorodheshwa na Wizara ya Afya katika vita dhidi ya janga la Covid-19.

Watu wanahimizwa kunawa mikono kila wakati kwa sabuni au jeli yenye kemikali kuua virusi vya corona, ambavyo vinasababisha ugonjwa wa Covid-19.

Mitungi yenye maji imewekwa katika kila lango la maeneo yanayotoa huduma kwa umma kama vile; benki, masoko, maduka ya jumla, vituo vya afya na vya polisi, miongoni mwa mengine.

Kabla kuingia kwenye matatu unahimizwa kuvalia maski na kutakasa mikono kwa jeli.

Hata hivyo, ulijua katika harakati za kufungua na kufunga tapu na pia kugusa kifaa kilichowekwa sabuni ya maji, kunaweza kukutia katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona? Mitungi na vifaa hivyo vinatumiwa na umma, na ni vigumu kutambua ni nani ana corona au hana.

Ni kufuatia hatari hiyo ambapo kijana James Nyakera, 27, kutoka Kaunti ndogo ya Mathioya, Kaunti ya Murang’a ameibuka na mtambo wa kipekee kunawa mikono.

Mtambo huo wa teknolojia ya kisasa na unaotumia nguvu za umeme au sola, hauhitaji kufungua au kufunga tapu.

Kijana Nyakera anasema unachohitaji ni kuelekeza mikono yako kwenye bomba la kutoa maji, kisha “mtambo utakuhudumia kuanzia mwanzo hadi mwisho”.

“Tapu ikihisi joto la mwili kupitia viganja vya mikono, mashine inatoa sabuni majimaji kwa muda wa sekunde kadhaa halafu inasitisha kutoa sabuni na kuruhusu maji kutoka mfululizo,” anaelezea.

Mashine hiyo na ambayo ikikumbatiwa italeta afueni kwa wananchi, ina sehemu ya kuweka sabuni majimaji na nyingine tofauti ya maji.

Isitoshe, barabaro huyo aliyejawa maarifa ya uvumbuzi anasema mtambo huo wenyewe ndio unasitisha maji kutoka, dakika kadhaa baadaye. “Hakuna unapotangamana kushika tapu au kifaa cha sabuuni. Unaepushia mtu hatari ya kuambukizwa corona kupitia harakati za kufungua na kufunga bomba la kuachilia maji,” asema.

Kulingana na Nyakera, ambaye ni gwiji wa masuala ya Sayansi na Teknoljia alianza utafiti wa mashine hiyo baada ya Kenya kutangaza kuwa mwenyeji wa Covid-19, ugonjwa ambao sasa ni kero la ulimwengu mzima. Kisa cha kwanza cha corona kiliripotiwa nchini mnamo Machi 13, 2020.

Anaiambia Taifa Leo Dijitali kwamba mashine hiyo inaundwa kwa mengi ya malighafi yaliyoko nchini; mtungi wa kuhifadhi maji na meza iliyojengwa kwa mbao au vyuma kuusitiri, na kuiweka mtambo unaofanikisha utoaji sabuni majimaji na maji.

“Maji humu nchini si kikwazo. Ni mtambo unaoundwa kwa kutumia malighafi tuliyonayo,” anasema.

Wakati wa mahojiano, alisema mashine hiyo imeidhinishwa na shirika la kutathmini ubora wa bidhaa nchini ndilo Kebs na pia idara ya afya Murang’a, ambapo amepata kibali kuingia sokoni.

Kijana huyu ambaye alihitimu Shahada ya Mawasiliano na Teknolojia (IT) kutoka Chuo Kikuu cha Mt Kenya (MKU) 2017 , anasema gharama ya kutengeneza mtambo mmoja ni kati ya Sh18, 000 – 22, 000. “Mashine moja ikiingia sokoni, haitakosa kuniingizia kati ya Sh27, 000 – 30, 000,” anadokeza.

Kikwazo kikuu cha Nyakera kuingiza uvumbuzi wake sokoni ni ukosefu wa fedha za kutosha kuunda mitambo mingi. Anasema hutegemea vibarua vya hapa na pale, na pia ufadhili wa mamake hasa kununua baadhi ya vifaa kutoka nje ya nchi. “Kuna vifaa ninavyoagiza kutoka Uchina na pia Korea,” anasema.

Nyakera anasema kuna vijana wengi mno nchini waliojaaliwa vipaji mbalimbali, ila kwa sababu ya ukosefu pesa na ufadhili kuvipalilia wanaishia kupotea.

“Vipaji wengi wamekufa moyo kwa sababu ya kukosa hamasisho na pia ufadhili kuonyesha umahiri wao, wajiendeleze kimaisha. Ndio maana baadhi yao huishia kutekwa na pombe na hata dawa za kulevya, kwa ajili ya msongo wa mawazo,” anafafanua.

Roger Wekhomba, mtafiti, anasema kwenye ziara yake katika mataifa mbalimbali Barani Afrika, amebaini changamoto zinazozingira vijana hapa Kenya zinawiana na nchi zingine Afrika, kwa kile anataja kama “ukosefu wa hamasa na ufadhili”.

“Masaibu yanayokumba vijana Kenya ni sawa na ya mataifa mengine Barani Afrika. Ukosefu wa fedha na wafadhili kuwainua, ikiwa ni pamoja na hamasisho linalopaswa kuendeshwa na asasi za serikali,” Wekhomba anasema.

Kulingana na mdau huyu ambaye pia hutoa mafunzo ya kuongeza mazao ya kilimo thamani, Ethiopia ndiyo nchi pekee Afrika inayojikakamua kuangazia masuala ya vijana hasa kuimarisha vipaji.

Mbali na kuibuka na mashine ya aina yake kunawa mikono, Nyakera pia amevumbua mtambo wa kuuza bidhaa majimaji (ATM) usiohitaji mhudumu kuwepo, mashine inayodhibiti kiwango cha joto kwenye kivungulio (green house), mtambo wa kuhesabu sarafu, mtambo wa kufunga na kufungua malango, wa king’ora kupiga mbiu kwenye makazi yanapovamiwa na wahalifu, miongoni mwa vumbuzi zingine.

You can share this post!

Mbappe kuuguza jeraha kwa muda mrefu

Uhuru anavyotumia mawaziri kufufua umaarufu wake nchini

adminleo