Michezo

Ripoti kuhusu kurejeshwa kwa michezo kutolewa

July 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

RIPOTI ya kamati ya watu 25 iliyoundwa na Wizara ya Michezo kutathmini mapendekezo ya wadau mbalimbali na kushauri Serikali kuhusu utaratibu wa kurejelewa kwa shughuli za michezo humu nchini sasa itawasilishwa kwa Waziri Amina Mohamed baada ya wiki moja.

Kamati hiyo iliyoko chini ya Katibu Mratibu wa Wizara ya Michezo, Hassan Noor Hassan, inajumuisha washikadau na wataalamu kutoka sekta na idara mbalimbali za serikali, mashirikisho ya michezo tofauti ya humu nchini na vyombo vya habari.

Ripoti hiyo ilitarajiwa kuwasilishwa mnamo Julai 10, lakini Amina akasema kwamba ilicheleweshwa baada ya kamati kutaka muda zaidi wa kufikia na kupata maoni ya washikadau wengi iwezekanavyo.

Ripoti itatoa mwelekeo kuhusu jinsi shughuli za michezo zilizoahirishwa mnamo Machi 2020 kwa sababu ya corona zitakavyorejelewa na kanuni ambazo wanamichezo na mashabiki wanastahili kuzingatia.

“Ripoti ililenga kushughulikia jinsi michezo itakavyokuwa ikiendeshwa kwa mafanikio chini ya masharti yaliyotolewa na Wizara ya Afya kuhusu namna ya kudhibiti maambukizi zaidi ya ugonjwa wa Covid-19,” akatanguliza Noor.

“Itatueleza ni watu wangapi wanastahili kushiriki na kuhudhuria aina mbalimbali ya michezo, kiwango cha kuhusishwa kwa idara nyinginezo za serikali na mchango ambao unafaa kutolewa na wizara hizo husika ili kufanikisha uendeshaji wa shughuli za michezo,” akaongeza Noor aliyekuwa akizungumza katika hafla ya kufunguliwa rasmi kwa uwanja wa Kericho Green ambao ulikarabatiwa kwa kima cha Sh100 milioni.

Uwanja huo ulioko katika Kaunti ya Kericho una uwezo wa kubeba zaidi ya mashabiki 20,000.

Baada ya kupokea ripoti, Amina anatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu jinsi wanamichezo watakavyorejea uwanjani na katika kumbi mbalimbali baada ya kusubiri kwa zaidi ya miezi minne.

Mnamo Julai 6, 2020, Rais Uhuru Kenyatta aliondoa marufuku yaliyozuia watu kuingia na kutoka katika Kaunti za Nairobi, Mombasa na Mandera na kuongeza kafyu kwa siku 30 zaidi. Aidha, mikusanyiko ya umma ilipigwa marufuku kwa siku 30 zaidi.

Ingawa hatua hiyo inatarajiwa kuwa kiini cha masharti mengine kulegezwa, huenda hilo lisitimie hasa ikizingatiwa wingi wa visa vya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Covid-19 tangu mipaka ya kaunti zote za humu nchini kufunguliwa.