Michezo

PSG washinda French Cup

July 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

PARIS Saint-Germain (PSG) walitawazwa mabingwa wa French Cup mnamo Ijumaa usiku baada ya kuwalaza Saint-Etienne 1-0 katika fainali iliyoshuhudia idadi ndogo ya mashabiki (5,000) wakiruhusiwa kuingia uwanjani Stade de France kuwatilia shime wanasoka wa timu zao.

Uwanja wa Stade de France una uwezo wa kubeba zaidi ya mashabiki 80,000 walioketi.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kuandaliwa nchini Ufaransa tangu msimu wa Ligi Kuu (Ligue 1) na Ligi ya Daraja la Kwanza (Ligue 2) kutamatishwa ghafla mnamo Aprili 2020 kutokana na mlipuko wa virusi vya homa kali ya corona.

Fowadi mzawa wa Brazil, Neymar Jr, aliwafungia PSG bao la pekee na la ushindi katika dakika ya 14. Kipindi cha kwanza cha fainali hiyo kilitawaliwa na hisia kali baada ya kiungo Loic Perrin kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kuchezea kivoloya chipukizi Kylian Mbappe kunako dakika ya 31.

Mbappe aliondolewa ugani kwa machela huku akitiririkwa na machozi. Alirejea katika eneo la wachezaji wa akiba baadaye akitembea kwa usaidizi wa mikongojo. Jeraha baya alilolipata sasa litamweka nje ya robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) itakayowakutanisha PSG na Atalanta ya Italia mnamo Agosti 12, 2020.

Bao la Neymar dhidi ya St Etienne liliwawezesha PSG kutia kapuni taji lao la 13 la French Cup. Ushindi huo uliwazolea pia kombe lao la pili msimu huu kwa kuwa walipokezwa ubingwa wa Ligue 1 baada ya msimu wa Ligi Kuu kutamatishwa rasmi mwishoni mwa Aprili 2020.

Licha ya kuumia kwa Mbappe, kocha Thomas Tuchel anaamini kwamba vijana wake wangali na uwezo wa kuwaangusha Atalanta na kupata hamasa itakayowachochea kutia kibindoni ufalme wa UEFA muhula huu.

“Kila mtu ana hofu. Yeyote ambaye aliona jinsi Mbappe alivyokabiliwa visivyo anastahili kuhofia. Kwa sasa tunasubiri ushauri wa daktari kujua lini atakafanyiwa upasuaji na atasalia mkekani kwa kipindi kipi,” akasema Tuchel katika kauli iliyosisitizwa na beki na nahodha Thiago Silva anayehusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua Arsenal mwishoni mwa msimu huu.