Mkenya Tyler Onyango kuchezea Everton msimu ujao
Na CHRIS ADUNGO
KIUNGO Tyler Onyango aliye na usuli wa Kenya, ametia saini mkataba wa kitaaluma na kikosi cha Everton nchini Uingereza.
Onyango, 17, aliingia katika sajili rasmi ya ‘The Toffees’ akiwa kitoto cha miaka minane pekee na kwa sasa ametuzwa kutokana na utajiri wa kipaji alichokidhihirisha uwanjani.
Sogora huyu aliyezaliwa na baba Mkenya na mama mzawa wa Uingereza sasa ametia saini mkataba wa miaka mitatu utakaomshuhudia akihudumu kambini mwa Everton hadi mwishoni mwa Juni 2023.
“Onyango ametia kidole kandarasi ya miaka mitatu na klabu ya wanasoka wazima wa Everton baada ya kuridhisha katika akademia alikowajibishwa sana katika timu ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 na 23. Kukwezwa kwake hadi kikosi cha kwanza kunatarajiwa kuongeza viwango vya ushindani kambini,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Everton.
Onyango alitegemewa sana katika mechi zilizopita za makinda wa Everton dhidi ya Crewe Alexandra na Fleetwood Town.
Katika mahojiano yake ya hivi karibuni na Nation Sports, nyota huyo alikiri kwamba atachangamkia sana fursa ya kuchezea timu ya taifa ya Harambee Stars kwa kuwa hajawahi kuwajibishwa na timu ya taifa ya Uingereza.
“Nimekuwa Kenya mara kadhaa, mara ya mwisho ikiwa 2018. Sitasita kuvalia jezi za Stars iwapo fursa hiyo itajipa kwa kuwa sijawahi kuchezea Uingereza licha ya kupangwa katika kikosi cha akiba cha wanasoka chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17,” akasema Onyango kwa kukiri kwamba hana umilisi wowote wa lugha za Kiswahili na Kiluo.