Michezo

Naishukuru City kwa kunikuza kisoka – David Silva

July 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO na nahodha David Silva, 34, amesema hakuna chochote anachoweza kukibadilisha katika kipindi cha miaka 10 ya mafanikio ndani ya jezi za Manchester City.

Nyota huyu wa zamani wa timu ya taifa ya Uhispania atasakata leo mechi yao ya 309 na ya mwisho katika soka ya Uingereza (EPL) akivalia sare ya Man-City dhidi ya Norwich City uwanjani Etihad.

Silva anatazamiwa kuagana rasmi na Man-City mwishoni mwa msimu huu na anahusishwa pakubwa na klabu za Inter Miami (Amerika), Real Betis (Uhispania), Vissel Kobe (Japan), Al-Duhail (Qatar) na AC Milan (Italia).

“Nikitazama nyuma na kuvuta fikira za kila kitu, siwezi kabisa kuamini iwapo ningeweza kufikia hapa nilipo na hivi nilivyo kitaaluma,” akasema.

Tangu aingie katika sajili rasmi ya Man-City baada ya kuagana na Valencia ya Uhispania mnamo 2010, Silva anajivunia kutia kimiani mabao 60 ya EPL na kuwashindia waajiri wake mataji matatu ya EPL, mawili ya Kombe la FA na matano ya EFL League Cup.

Ni matumaini ya kocha Pep Guardiola kwamba Silva atakamilisha kipindi cha kuhudumu kwake kambini mwa Man-City kwa kuzoa ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) wakati wa fainali itakayoandaliwa jijini Lisbon, Ureno mnamo Agosti 2020.

“Iwapo ningalikuwa na fursa ya kujishauri kuhusu mambo ya kufanya nikiwa mchezaji wa Man-City, ningalitaka kufanya chote nilichofanya na jinsi nilivyofanya kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita ugani Etihad,” akasema.

Silva anakuwa mwanasoka wa tano baada ya Yaya Toure, Pablo Zabaleta, Joe Hart na Vincent Kompany kuondoka Etihad kutoka kwa kikosi kilichowanyanyulia Man-City ufalme wa EPL mnamo 2012 baada ya kusubiri kwa miaka 44. Kati ya wanasoka hao, ni mvamizi Sergio Aguero pekee atakayesalia baada ya Silva kubanduka.

Guardiola amemtaka Silva kurejea baadaye uwanjani Etihad kushiriki mechi itakayowapa mashabiki jukwaa zuri zaidi la kumuaga kirasmi kabla ya kuwazia kurejea upya katika kikosi hicho kudhibiti mikoba iwapo atapania kujitosa katika ulingo wa ukufunzi.

Silva amechangia jumla ya mabao 95 tangu awajibishwe kwa mara ya kwanza kambini mwa Man-City mnamo Agosti 2010.

Katika umri wake wa miaka 34 na siku 189, ndiye mwanasoka wa tatu mkongwe zaidi katika historia ya EPL kuwahi kuchangia zaidi ya mabao 10 katika msimu mmoja baada ya Dennis Bergkamp, 35, (2004-05, Arsenal) na Paolo Di Canio, 35, (2003-04, Charlton Athletic).